IQNA

Waislamu Marekani washambuliwa baada ya ushindi wa Trump

18:03 - November 11, 2016
Habari ID: 3470666
IQNA-Kumeshuhudiwa wimbi la hujuma dhidi ya Waislamu kote Marekani baada ya Donald Trump kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais siku ya Jumanne.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, kuna matukio kadhaa ya kushambuliwa wanawake Waislamu waliokuwa wamevaa vazi la stara la Hijabu huku maandishi ya kibaguzi yakiandikwa katika misikiti.

Kwa mujibu Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR), ambalo hutetea haki za Waislamu, mbali na wanawake Waislamu kushambuliwa pia kumeshuhudiwa hujuma dhidi ya watoto Waislamu.

"Hii ni natija ya chuki dhidi ya Uislamu kuwa sera rasmi kama ambavyo tumeshuhudia miezi ya hivi karibuni katika kampeni za uchaguzi wa rais,” amesema msemaji wa CAIR Ibrahim Hooper. Aidha amesema ni jukumu la Trump kulaani ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu. Hadi sasa Trump au wapambe wake hawajatoa taarifa yoyote kuhusu kuongezeka hujuma dhidi ya Waislamu Marekani.

Wakati wa kampeni zake, Trump aliwahi kusema kuwa, endapo atachaguliwa kuwa Rais wa Marekani atawapiga marufuku Waislamu kuingia nchini humo.

Matamshi hayo ya kibaguzi ya Trump yalilaaniwa kote duniani hususan katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Siku ya Jumatano, mwanafunzi wa kike aliyekuwa amevaa Hijabu katika Chuo Kikuu cha San Diego alihujumuiwa na vitu vyake kuibiwa ambapo waliomhujumu walitoa matamshi ya kumuunga mkono Trump huku wakitoa nara dhidi ya Waislamu. Katika Chuo Kikuu cha San Jose California siku ya Jumatano, mwanamke Mwislamu alivuliwa Hijabu yake wakati akitembelea katike eneo la kuegesha magari.

Katika upande mwingine Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu katika Chuo Kikuu cha New York pia imelaani kitendo cha kuchorwa jina la Donald Trump kwenye mlango wa eneo la kuswalia ndani ya chuo hicho. Itakumbukwa kuwa akiwa katika kampeni zake za uchaguzi, rais mteule wa Marekani, Donald Trump aliweka wazi misimamo yake iliyo dhidi ya Waislamu na kutoa wito wa kutumiwa mbinu za dikteta wa zamani wa Ujerumani Adolph Hitler dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.

Wanawake Waislamu nchini Marekani sasa wametakiwa na familia zao kubakia majumbani ili kujiepusha na mashambulizi na hujuma mbalimbali.

3545045

captcha