IQNA

Mabasi Uingereza yapambwa kwa Jina la Mtume Muhammad SAW na Ujumbe wa Amani

15:53 - December 07, 2016
Habari ID: 3470722
IQNA-Mabasi kadhaa nchini Uingereza yamepambwa kwa jina la Mtume Muhammad SAW na ujumbe wake wa Amani kwa munasaba wa kuwadia sherehe za Mawlid ya Mtukufu Huyo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, kampeni hiyo imezinduliwa kwa munasaba wa kuanza Mfungo Sita Rabbiul Awwal, mwezi ambao Waislamu wanasherehekea Mawlid (kuzaliwa) ya Mtume Muhammad SAW.

Kampeni hiyo ya wiki nne ambayo inadhaminiwa na Waislamu inajumuisha mabasi 128 ya umma kote Uingereza ambayo yatakuwa na matangazo yenye ujumbe wa kheri na fanaka na amani kwa wote.

Mabasi hayo yana ujumbe usemao "Enyi Watu, Enezeni Amani na Muwalishe Watu” na kando ya maneno hayo kuna jina la Mtume Muhammad SAW ililopambwa kwa waridi.

Walioandaa ujumbe huo wanasema lengo ni kuwafikia watu wote Uingereza kwa munasaba wa kipindi hiki ambacho Waislamu wanaadhimisha Mawlid ya Mtume SAW na Wakristo wanasherehekea uzawa wa Nabii Issa (Yesu) AS katika msimu wa Krismasi.

Kilele cha kampeni hiyo kitakuwa ni tarehe 17 Disemba mwaka 2016 ambapo kutakuwa na Sherehe za Kimataifa za Mawlid ambazo zitafanyika katika miji kadhaa duniani lengo likiwa ni kuwahimiza Waislamu kutoa mchango mzuri na kueneza amani katika jamii zao.

Sherehe za Kimataifa za Mawlid zinafanyika kwa mwaka wa tano mfululizo ambapo Waislamu hubeba maua ya waridi yenye ujumbe wa Mtume Muhammad SAW kuhusu amani, mapenzi na rehema hufikishwa kwa jamii katika miji mikubwa na midogo maeneo mbali mbali duniani. Washiriki watagawa maua ya waridi na switi kwa umma lengo likiwa ni kueneza ujumbe wa Mtume Mtukufu wa Uislamu kuhusu amani, mapenzi na matumaini kwa jamii yote ya wanadamu.

Nchini Uingereza waliojitolea kushiriki katika kampeni hiyo ya Miladun Nabii SAW watajitokeza katika maeneo 125 nchini humo huku baadhi ya sherehe hizo zikifanyikwa kwa wakati moja. Kati ya miji ya Uingereza ambazo kutafanyika sherehe kubwa za Mawlid ni London, Birmingham, Manchester, Nottingham, Sheffield, Coventry, Luton and Glasgow.

Halikadhalika Waislamu watamkabidhi Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May ua la waridi na ujumbe wa amani katika ofisi yake huko 1O Downing Street mjini London katika kilele cha sherehe hizo ambazo zitafanyika pia Marekani, Canada, Australia na maeneo mengi ya Ulaya Magharibi.

Hafla hizo zimeandaliwa na Jumuiya ya As Siraat ambayo inasimamiwa na Waqfu wa Hazrat Sultan Bahu yenye makao yake Birmingham Uingereza. Msomo mwandamizi katika Jumuiya ya As Sirat Sheikh Mohammad Amar anasema, "kuwadia mwezi wa Disemba si kuwa ni muhimu kwa jamii ya Wakristo, bali pia mwaka huu mwezi huo umesadifiana na kuwadia mwezi mtukufu wa Kiislamu wa Rabi ul Awwal.”

Naye mmoja wa waandalizi wa sherehe hizo Abdul Rehman Tobin anasema ni jambo la kusikitisha kuwa ujumbe halisi wa Uislamu umepotoshwa kutokana na mazingira ya sasa ya hofu lakini kwa kuwazawadia wananchi maua ya waridi na kadi zenye ujumbe wa amani, tunawapa watu fursa ya kuzungumza na Waislamu na kuuliza maswali ili kuondoa dhana potovu zilizopo.

3461584

captcha