IQNA

Chuo Kikuu cha Sarajevo kufungwa wakati wa Sala ya Ijumaa

18:35 - December 31, 2016
Habari ID: 3470770
IQNA-Chuo Kikuu cha Sarajevo nchini Bosnia Herzegovina kimetangaza kitakuwa kikufungwa adhuhuri wakati wa Sala ya Ijumaa ili Waislamu chuoni hapo wahudhurie sala hiyo ya kila wiki.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Chuo Kikuu cha Sarajevo kimeanza kutekeleza mpango huo Ijumaa ya jana ambapo masomo yalifungwa kwa muda wa saa moja na nusu ili kuwawezesha Waislamu kupata nafasi ya kutosha ya kushiriki katika Sala ya Ijumaa.

Ingawa chuo hicho huwa hakina masomo Jumamosi na Jumapili, siku ambazo ni za ibada kwa Wakristo Wakatoliki na Waorthodoxi nchini humo, lakini Milorad Dodic Rais wa Jamhuri ya Srpska katika Shirikisho la Bosnia Herzegovina amelaani hatua hiyo.

Dodic pia amelaani hatua ya wakuu wa mji wa Sarajevo kupiga marufuku pombe wakati wa sherehe za kuukaribisha mwaka mpya wa miladia. Vyama vya mrengo wa kushoto na vyama vya kiliberali nchini humo pia vimepinga hatua ya chuo kikuu hicho kufunga shughuli zake wakati wa Sala ya Ijumaa. Hatahivyo Chuo Kikuu cha Sarajevo kimesema hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la "kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa kuabudu"

Karibu nusu ya watu wote milioni 3.5 nchini Bosnia Herzegovina ni Waislamu.

Waislamu wa Bosnia wamekuwa wakikumbwa na masaibu kwa muda mrefu kutokana na kubaguliwa katika nchi hiyo ya Ulaya kusini.

Itakumbukwa kuwa Katikati ya mwezi Julai mwaka 1995 katika vita vya Bosnia, majeshi ya Serbia yakiongozwa na Jenerali Ratco Mladic yaliwauwa kwa halaiki Waislamu wanaokaribia 8,000 wa Srebrenica wakiwemo wanawake na watoto, na mauaji hayo kunahesabiwa kuwa makubwa zaidi kutokea barani Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia.

3461821


captcha