IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Maadui wa Iran ni Marekani, Uingereza, mabepari wa kimataifa na Wazayuni

22:36 - January 08, 2017
Habari ID: 3470789
IQNA-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, "maadui asili wa Iran huru na iliyostawi," ni Marekani, Uingereza, mabepari wa kimataifa na Wazayuni.
Maadui wa Iran ni Marekani, Uingereza, mabepari wa kimataifa na Wazayuni
Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasmea hayo leo Jumapili hapa mjini Tehran wakati alipokutana na maelfu ya wakaazi wa Qum na kuongeza kuwa maadui asili wa kigeni si nara bali ni ukweli wenye nyaraka na ushahidi. Ameongeza kuwa: "Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayataja kuwa eti ni 'mwenye muamala mwema' katika barua yake ya kuaga ameishauri serikali ijayo nchini humo, 'ichukue hatua kali dhidi ya Iran na iendeleze vikwazo kwani kwa hatua hizo kali itaweza kulegeza misimam ya Iran." Amesema huyu adui mwenye kutabasamu hana tafauti hata kidogo na yule aliyeitaja Iran kuwa mhimili wa shari.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uadui wa 'Waingereza' na kusema: "Uingereza ni mkoloni mkongwe aliyechakaa na sasa kwa mara nyingine amekuja katika Ghuba ya Uajemi kwa lengo la kuzitumia nchi za eneo hili kwa maslahi yake na ni kwa sababu hii ndio maana katika hali ambayo yeye ndiye tishio halisi anadai kuwa eti Iran ndiyo tishio."
Kiongozi Muadhamu ameendelea kusema kuwa: "Uingereza inapanga na kuchukua maamuzi kwa ajili ya nchi za eneo hili ikiwemo Iran na moja ya malengo yake ni kuzigawa vipande vipande nchi za Iraq, Syria, Yemen na Libya na ina nia hiyo hiyo kuhusu Iran lakini kwa kuhofia fikra za umma, nchini Iran hailitaji lengo hilo wazi wazi."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Waingereza wanasema wanatekeleza mpango kwa ajili ya vizingiti na vikwazo vya baada ya mapatano ya nyuklia ya Iran na pia wanatoa mafunzo na kuwapa silaha wenyeji wa eneo hili wakiwemo walioko Iran ili waweze kutoa pigo kwa mfumo wa Kiislamu na taifa.
Ayatullah Khamenei ameashiria mpango na njama za majopo ya kifikra  ya Marekani na Uingereza katika kukabiliana na "dini ya kisiasa'  huku wakiwa na mpango wa 'kutenganisha dini na siasa na kusema: "Wanalenga kuhakikisha kuwa dini inabakia ndani ya misikiti na ndani ya nyumba na kuifanya dini iwe jambo la mtu binafsi huku wakipinga dini ambayo inaenda sambaba na hatua za kivitendo katika massuala ya uchumi na siasa. Aidha wanataka dini ambayo inasalimu amri mbele ya adui."
Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, adui anaogopa dini ambayo ina uwezo wa kusimamia masuala ya serikali, uchumi, siasa, nguvu, jeshi na mfumo wa kifedha na kiidara. Kwa msingi huo amesema maarifa sahihi ya dini ni yale ambayo hayatenganishi dini, maisha na siasa.
Kiongozi Muadhamu ameashiria namna adui hakulifahamu vizuri taifa la Iran katika fitina za mwaka 2009 na kusema fitina hizo ni mfano wa wazi wa makosa katika mahesabu ya adui. Ameongeza kuwa katika mwaka huo kwa kuzusha fitna mwaka huo, adui alidhani anaelekea kupata mafanikio lakini ghafla wananchi wakaibua hamasa kubwa ya 9 Dei ambayo ilishambihiana na ile ya 19 Dei. 
Katika siku hii ya kihistoria ya tarehe 19 Dei 1356 mwaka wa Kiirani, iliyosadifiana na tarehe 9 Januari, 1978, kuliibuka harakati ya Chuo cha Kidini (Hawza) cha Qum ya kupinga kuchapishwa makala iliyomvunjia heshima Imam Khomeini MA iliyochapishwa na gazeti la Etelaat la nchini Iran. Maandamano ya kumpinga mtawala wa kiimla Shah Pahlavi yalifanyika kote Iran wakati huo. 
 
 
captcha