IQNA

Mazishi ya Ayatullah Hashemi Rafsanjani mjini Tehran

0:22 - January 11, 2017
Habari ID: 3470791
IQNA-Mwili wa marehemu Ayatullah Hashemi Rafsanjani, Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran umezikwa Jumanne katika haram ya mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini (MA) kusini mwa Tehran

Mapema asubuhi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ndiye aliyeongoza Sala ya Jeneza (Maiti) ya marehemu Ayatullah Rafsanjani katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Tehran.

Viongozi wa ngazi za juu za nchini, wakiwemo wa serikali na vikosi vya ulinzi pamoja na mabalozi kadhaa wa nchi za nje walioko mjini Tehran walishiriki kwenye shughuli ya maziko ya Sheikh Hashemi Rafsanjani.

Mwili wa Sheikh Hashemi Rafsanjani, ulisindikizwa na mamia ya maelfu ya waombolezaji wa Iran ya Kiislamu kutoka Chuo Kikuu cha Tehran kuelekea haram toharifu ya Imam Khomeini (MA). Inakadiriwa kuwa takribani watu milioni tatu walihudhuria mazishi na maziko ya Ayatullah Rafsanjani.
Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran aliaga dunia Jumapili usiku kutokana na matatizo ya moyo katika hospitali moja ya mjini Tehran.

Habari ya kifo cha Ayatullah Rafsanjani aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 82 si tu kwamba imelishtua taifa la Iran bali shakhsia na wanasiasa mashuhuri kote duniani pia wamepatwa na mshtuko kutokana na kifo hicho.

Rafsanjani alitumia sehemu kubwa ya umri wake katika mapambano na kuwazindua na kuwahamasisha wananchi dhidi ya utawala wa kifalme nchini Iran na katika njiahiyo alistahamili mashaka, mateso na taabu nyingi katika jela na korokoro za utawala wa kifalme wa Shah. Jitihada na juhudi zake kubwa na roho yake ya kimapinduizi vilimuweka katika safu ya kwanza ya vinara wa harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kadiri kwamba, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu nchiniIran, Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei anasema alikuwa egemeo la kuaminiwa kwa watu wote walioshirikiana naye.

Nyota ya Ayatullah Hashemi Rafsanjani iling'ara zaidi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini kwa kuchukua majukumu mazito wakati wa kipindi cha vita vya kujitetea kutakaifu, katika Bunge wakati alipokuwa Spika kwa vipindi viwili, wakati alipochukua jukumu la kuongoza serikali kama Rais wa nchi na katika nafasi yake ya mwisho kama Mkuu wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran. Daima alisisitiza sana katika matamshi na hotuba zake za Swala ya Ijumaa juu ya udharura wa kuimarishwa umoja wa Kiislamu na kuondoa mifarakano na uhasama. Ayatullah Rafsanjani alikuwa mtu wa siasa na kuchapakazi na alielewa vyema mahitaji ya nyakati na zama mbalimbali.

Ingawa Ayatullah Rafsanjani, ambaye alihesabiwa kuwa moja kati ya nguzi za Mapinduzi ya Kiislamu, ameaga dunia, lakini jitihada, jihadi na turathi zake kubwa zitabakia hai siku zote kwa wananchi wanamapinduzi katika Jamhuri ya Kiislamu na kote duniani.

3561451


azishi ya Ayatullah Hashemi Rafsanjani mjini Tehran

captcha