IQNA

Rais wa Kenya aomboleza kifo cha mwanazuoni wa Kiislamu

18:49 - February 28, 2017
Habari ID: 3470872
IQNA: Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya ameomboleza kifo cha mwanazuoni maarufu wa Kiislamu Sheikh Hassan Suleiman aliyefariki dunia Jumapili.

Katika taarifa, Rais Kenyatta amepongeza jitihada za Sheikh Suleiman za kuelimisha jamii ya Waislamu katika uhai wake wakati akiwa Naibu Mwenyekiti Kitaifa wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu Kenya. Rais Kenyatta amemtaja marehemu Sheikh Suleiman, ambaye pia aliwahi kuwa naibu msajili wa vyeti vya ndoa na talaka mjini Mombasa, kuwa mwanazuoni ambaye aliongoza jitihada za kukabiliana na misimamo mikali ya kidini mbali na kuwa mwanazuoni mwenye kujitolea.

Halikadhalika Rais wa Kenya amesema Sheikh Suleiman alikuwa na nafasi muhimu katika kutatua migogoro ya watu binafsi na makundi na katika kipindi chote cha maisha yake alifungamana na amani na umoja kwani aliamini kuwa wanadamu wote pasina kujadili dini au kabila wanapaswa kuishi kwa amani.

Rais wa Kenya amesema Sheikh Suleiman ameacha pengo kubwa na daima atakumbukwa kwa mchango wake wa kuleta umoja katika jamii ya Waislamu na Kenya kwa ujumla. Rais Uhuru Kenyatta alimaliza ujumbe wake kwa kuashiria sehemu ya aya ya 145 Surat al Baqara katika Qur'ani Tukufu isemayo: Inna lillahi wa Inna Ilayhi Raji'un yaani Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.

Sheikh Hassan Suleiman aliaga dunia Jumapili nyumbani kwake mjini Mombasa katika eneo la Guraya. Katibu Mwandalizi wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Kenya Sheikh Mohammed Khalifa amesema Sheikh Suleiman alikuwa anaugua moyo na figo kwa muda mrefu na hata aliwahi kuenda India kwa ajili ya matibabu. 

Rais wa Kenya aomboleza kifo cha mwanazuoni wa Kiislamu

Rais Kenyatta (kushoto) akiwa na marehemu Sheikh Suleiman enzi za uhai wake

Marehemu Sheikh Suleiman, ambaye pia alikuwa Imamu katika Masjid Tauba eneo la Kisauni, alizikwa Jumapili usiku katika Makaburi ya Seif Halua baada ya Sala ya Jeneza katika Masjid Noor, Bondeni. Marehemu Sheikh Suleiman alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa Baraza la Maimamu na Wahubiri wa Kiislamu Kenya.

captcha