IQNA

Mashindano ya Qur'ani Iran yalenga kuleta umoja wa Waislamu, mafanikio kwa mfumo wa Kiislamu

19:46 - April 16, 2017
Habari ID: 3470936
TEHRAN (IQNA)-Mashindano ya kitaifa na kimataifa ya Qur'ani ni kati ya mafanikio makubwa ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na yanalenga kuleta umoja wa Waislamu.

Hayo yamesemwa na Hujjatul Islam Ali Mohammadi, Mkuu wa Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri Iran wakati akizungumza na waandishi habari Jumapili mjini Tehran. Mkutano huo umeitishwa kutoa maelezo kuhusu maandalizi ya Mashindano ya 34 ya Qur'ani Tukufu ya Iran yatakayoanza Aprili 19 hapa Tehran.

Hujjatul Islam Mohammadi amesema kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran yataendelea kwa muda wa siku sita na kuwaleta pamoja washiriki kutoka nchi 83 duniani. Amesema mashindano ya mwaka huu yatakuwa maalumu kwani kwa wakati moja kutafanyika mashindano matano ya kimataifa ambapo mbali na yale ya kawaida ya wanaume kutakuwa pia na mashindano maalumu ya wanawake, watu wenye ulemavu wa macho, ya wanachuo wa vyuo vya dini na pia mashindano ya wanafunzi wa shule.

Aidha Mkuu wa Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri Iran amesema mashindano ya mwaka huu pia yatakuwa na washiriki 276 na kuongeza kuwa wananchi wote wanakaribishwa kutizama mashindano .

Hujjatul Islam Muhammadi amesema kauli mbiu ya mashindano ya kimatiafa ya Qur'ani nchini Iran ni "Kitabu Kimoja Umma Moja" na kuongeza kuwa nara hii imetokana na mafundisho ya  Qur'ani Tukufu. Amesema kuwa, nara hiyo inalenga kuleta umoja miongoni mwa Waislamu na ni kati ya malengo muhimu ya mashindano ya Qur'ani yanayoandaliwa na Iran.

Mkuu wa Shirika la Waqfu na Mambo ya Kheri Iran amesema kati ya maudhui nyingine muhimu katika mashindano ya Qur'ani ni namna ya kukabiliana na madola ya kiistikbari na kibeberu na kuongeza kuwa ni muhimu kumfahamu adui na njama zake.

Amesema pia maudhui nyingine muhimu ya mashindano ya kimataifa ya Qur'ani mwaka huu ni kuhimiza mtindo wa maisha ya Kiislamu na kwamba maudhi zitakazojadiliwa ni 'Familia na Qur'ani' na pia mtazamo  wa Uislamu kuhusu 'Maisha ya Wanandoa' na 'Ndoa' .

Kwa mujibu wa Hujjatul Islam Muhammadi, mbali na mashindano ya Qur'ani pia kutakuwa na 'Kongamano la 10 la Utafiti wa Qur'ani' na tayari Makala 421 zimepokelewa kwa ajili ya kongamano hili ambapo kuna makala 64 kutoka nchi 20 za kigeni.

3590034
captcha