IQNA

Mkenya afika fainali mashindano ya kuhifadhi Qur'ani nchini Iran

16:39 - April 22, 2017
2
Habari ID: 3470945
TEHRAN (IQNA) –Raia wa Kenya amefika fainali za Mashindano ya 34 ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur'ani Tukufu yanayofanyika nchini Iran.

Katika mahojiano maalumu na mwandishi wa IQNA, Ustadh Haitham Sagar Ahmad mwenye umri wa miaka 26 anasema alianza kuhifadhi Qur'ani akiwa na umri wa miaka 10.

Anabainisha zaidi kuhusu chanzo cha motisha katika kuhifadhi Qur'ani kwa kusema: "Wakati nilipoanza kuhifadhi Qur'ani, nilikitizama kitabu hicho kitukufu kama sehemu ya maisha yangu kwani wazazi wangu walikuwa wamenipa nasaha kuwa, Qur'ani inatoa muongozo bora wa maisha."

Anaongeza kuwa, baada ya kuhifadhi kikamilifu Qur'ani Tukufu aliweza kudiriki vyema kuhusu umuhimu wa kitabu hicho kitukufu kama muongozo kamili wa maisha. "Siwezi tena kujiweka mbali na Qur'ani na Mitume waliotajwa katika Qur'ani ni kigezo bora cha maisha yangu," anasema Ustadh Safar.

Hafidh huyu wa Qur'ani kutoka Kenya anasema wazazi wake walikuwa na nafasi muhimu katika kumshawishi ahifadhi Qur'ani. Anaongeza kuwa: "Katika kudiriki vyema Qur'an nimeshiriki katika darsa maalumu za tafsiri na tarjama ya Qur'ani kwani pasina kufahamu maana ya Qur'ani hauwezi kufaidika ipasavyo na kitabu hiki kitukufu."

Ustadh Haitham Sagar Ahmad anasema ameshiriki katika mashindano kadhaa ya kimataifa ya Qur'ani katika nchi kama vile Bahrain, Libya, Misri na Tanzania ambapo katika mashindano ya Tanzania alishika nafasi ya pili na baada ya hapo akapata fursa ya kushiriki katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani nchini Iran.

Mkenya huyu aliyefika fainali za mashindano ya kimataifa ya Qur'ani nchini Iran anafafanua kuhusu nara ya mashindano ya mwaka huu ambayo ni 'Kitabu Kimoja, Umma Moja', na kusema: "Katika mashindano haya nimeona nara hii ikitekelezwa kivitendo kwani Waislamu wa madhehebu za Sunni na Shia wanashiriki pamoja chini ya kivuli cha Qur'ani na hivyo kuhifadhi umoja wao."

Ustadh Sagar anasema kwa kufuata mafundisho ya Qur'ani, Waislamu wanaweza kufikia malengo ya juu maishani na bila shaka lengo la juu zaidi ni kumridhisha Mwenyezi Mungu.

Kuhusu harakati zake za Qur'ani nchini Kenya anasema: "Kwa kuzingatia kuwa Kenya si nchi ya Kiislamu na wala serikali haifadhili harakati za Qur'ani, tuna jitihada binafsi na kwa mfano mimi nina wanafunzi wengi ninaowafunza kuhifadhi Qur'ani."

Ustadh Sagar anawanasihi vijana Waislamu kufuata mafundisho ya Qur'ani na kuimarisha ufahamu wao wa kitabu hiki kitukufu kwani ndio muongozo kamili wa maisha.

Huku akisifu ukarimu wa Wairani walioandaa mashindano ya Qur'ani, hafidh huyu kutoka Kenya ameelezea matumaini yake kuwa atashika nafasi ya kwanza huku akitumai kualikwa tena katika mashindano mengine nchini Iran. Kwa ujumle kuna washiriki 16 waliofanikiwa kuingia fainali katika kitengo cha kuhifadhi  katika mashindano ya mwaka huu ya kimataifa ya Qur'ani nchini Iran. Mbali na mshiriki kutoka Kenya wengine waliofika fainali ni kutoka Iran, Syria, Bangladesh, Afghansitan, Niger, Yemen, Uganda, Chad, Tajikistan, Nigeria, Indonesia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Algeria, Iran na Ujerumani. Washiriki hao wamefika fainali baada ya kushindana na wenzao katika mashindano hayo yaliyofunguliwa rasmi Jumatano Aprili 19.

Mashindano yataendelea kwa muda wa siku sita hapa Tehran, hadi tarehe 27 Rajab, katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini MA ambapo kuna washiriki 276 kutoka nchi 83 duniani.

3591898
Imechapishwa: 2
Inatathminiwa: 0
Haiwezi kuchapishwa: 0
suwaka isack mbwana
0
0
Inshallah ustadh sagar mungu akuwezeshe ushinde mashindano hayo amin"""
layla
0
0
Yarabbi akufanyie wepesi
captcha