IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Waislamu wafahamu sababu za uadui wa Marekani, Israel dhidi Uislamu na Iran

23:43 - April 25, 2017
Habari ID: 3470951
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Marekani na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zinaipinga Iran ya Kiislamu kwa kuwa Uislamu umedhihiri nchini hapa na ndio unaozuia tamaa zao
Kiongozi Muadhamu ameyasema hayo Jumanne ya leo mjini Tehran alipokutana na hadhara ya viongozi wa serikali na mabalozi wa nchi za Kiislamu kwa mnasaba wa siku ya kubaathiwa Mtukufu Mtume Muhammad SAW. Katika hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuelewa kiini cha uadui wa waistikbari dhidi ya Uislamu kuwa ni wajibu wa viongozi wa nchi za Kiislamu na kubainisha kuwa, serikali za Kiislamu ni lazima zitambue kwamba lengo la Marekani kushirikiana na nchi moja ya Kiislamu na kujenga uadui na nyengine ni kuzuia kupatikana umoja wa Ulimwengu wa Uislamu na kuzuia kuwepo uelewa wa pamoja wa Waislamu kuhusu maslahi ya jamii za Kiislamu.

Uwezo wa Uislamu kuleta maendeleo

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, uwezo usio na mbadala wa Uislamu katika kuleta maendeleo na ustawi wa jamii za mwanadamu, uwezo wake wa kujenga ustaarabu uliochanganya pamoja umada na umaanawi na pia uwezo wa Uislamu katika kukabiliana na dhulma na uchupaji mipaka, ni sababu kuu ya uadui wa mabeberu dhidi ya dini ya Kiislamu na akafafanua kwamba kuunda makundi ya kigaidi kwa jina la dini hii na kuchochea mifarakano baina ya nchi za Kiislamu, ni njama zinazotekelezwa na Marekani na utawala haramu wa Israel.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kwamba, wavamizi kwa kushirikiana na baadhi ya nchi za eneo na katika kuendeleza kazi hiyo wanafanya njama za kuionyesha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran au Ushia kuwa ni adui wa nchi hizo za eneo na kwamba, hata hivyo Waislamu wote wanapaswa wafahamu kuwa, umoja na kusimama imara kukabiliana na watumiaji mabavu hao, ndio njia pekee ya kupata maendeleo Ulimwengu wa Kiislamu.

Atakayejaribu kuihujumu Iran atajidhuru mwenyewe

Kadhalika Ayatullahil-Udhma Sayyid Ali Khamenei ameashiria siasa za vitisho za viongozi wote wa Marekani waliopita na wa sasa katika kupinga na kufanya uadui dhidi ya taifa la Iran na kusema kuwa, mienendo hiyo inaonyesha nia mbaya ya viongozi wa mirengo yote ya kisiasa nchini Marekani na kwamba, wakati wowote ambao Wamarekani wangeweza kutoa pigo dhidi ya Iran basi wasingechelewa kufanya hivyo. Kiongozi Muadhamu amewaonya viongozi wa Marekani kwamba, mtu yeyote atakayejaribu kuivamia Iran, bila shaka atajidhuru yeye mwenyewe. Katika sehemu nyingine Kiongozi Muadhamu amewahutubu wagombea urais nchini Iran kwa kuwataka, wawaahidi wananchi kwamba katika kuiletea maendeleo nchi, ustawi wa kiuchumi na kuwatatulia wananchi matatizo yao mtazamo wao wa kufikia malengo hayo hautokuwa wa kutegemea nje ya mipaka ya Iran.

Rais Rouhani: Waislamu wamfuate Mtume SAW kujinasua

Kabla ya Kiongozi Muadhamu, Rais Hassan Rouhani alisema kuwa, utawala wa kidini unaotokana na matakwa ya wananchi ni moja ya zawadi ya kubaathiwa Mtume wa Uislamu na kwamba Ulimwengu wa Kiislamu hii leo unakabiliwa na ukatili, ugaidi, ukufurishaji, machafuko na ukosefu wa usalama. Amesema kuwa hii leo kwa kufuata somo la kubaathiwa Mtume wa Uislamu, nchi za eneo la Mashariki ya Kati na za Kiislamu zinatakiwa kujinasua na matatizo, ukosefu wa usalama na machafuko.

3589908


captcha