IQNA

Mwanazuoni mwingine wa Kiislamu Bahrain akamatwa

16:52 - April 29, 2017
Habari ID: 3470958
TEHRAN (IQNA) –Utawala wa kiimla wa Bahrain umemtia mbaroni mwanazuoni mwingine wa Kiislamu huku ukandamizaji mkubwa wa wapinzani ukiendelea katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.

Taarifa zinasema wanajeshi wa Bahrain waliokuwa wamefunika nyuso zao walivamia nyumba ya Sheikh Abdul-Zahra Karbabadi katika kijiji cha Karbabad kaskazini mwa nchi hiyo siku ya Ijumaa. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu alikamatwa pamoja na mke wake na wanashikiliwa eneo lisilojulikana.

Aidha wanajeshi wa utawala wa Aal Khalifa walikihujumu kijiji cha Karrana na kumkamata dada yake mwanazuoni huyo.

Agosti 10 2016, wanajeshi wa Bahrain waliwakamata wanazuoni wanne wa Kiislamu waliotambuliwa kama Sheikh Imad al-Sho’leh, Sheikh Aziz al-Khazran, Sheikh Monir Ma’tooq na Sayyid Mohammad al-Ghoraifi katika kijiji cha Diraz yapata kilomita 12 kutoka mji mkuu Manama. Wanakabiliwa na tuhuma za kupanga njama za kuupindua utawala wa kifalme.

Aidha Julai 25 mwaka 2016 wanajeshi wa Bahrain pia waliwakamata wanazuoni wengine wa Kiislamu ambao ni Sayed Yassin al-Mosawi na Sheikh Jassim al-Kayyat katika kijiji cha Diraz kwa tuhuma za kushiriki katika mgomo nje ya nyumba ya mwanazuoni mwingine maarufu wa Kiislamu Sheikh Issa Qassim ambaye utawala wa Bahrain umempokonya uraia kwa ajili ya misimamo yake ya kutetea haki na uadilifu.

Hayo yanajiri wakati ambao, mahakama ya utawala wa Bahrain Disemba mwaka jana ilimhukumu mwanazuoni mwingine wa Kiislamu kifungo cha miaka tisa jela. Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kitaifa ya al Wifaq ambayo imepigwa marufuku nchini humo alikabiliwa na mashtaka ya kuupinga utawala wa ukoo wa Aal Khalifa.

Malalamiko na maandamano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya watawala dhalimu wa nchi hiyo yamekuwa yakiendelea tokea tarehe 14 Februari 2011. Tokea mwanzoni mwa maandamano hayo watawala wa ukoo wa Aal Khalifa wamekuwa wakitekeleza mbinu tofauti za kupambana na wapinzani.

3462692
captcha