IQNA

UAE yaingiza siasa mashindano ya Qur’ani, wawakilishi wa Qatar, Somalia watimuliwa

12:16 - June 13, 2017
Habari ID: 3471018
TEHRAN (IQNA)-Kufuatia nchi kadhaa za Kiarabu zikiongozwa na Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE kukata uhusiano na Qatar, washiriki wa Qatari na Somalia wametimuliwa katika mashindano ya Qur’ani ya Dubai.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, UAE imechukua hatua ya kibaguzi na iliyojaa taasubi kinyume cha mafundisho ya Kiislamu na kuwafukuza wawakilishi wa Qatar na Somalia katika Mashindano ya 21 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Dubai ambayo ni maarufu kama Zawadi ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Dubai (DIHQA).

Ikumbukwe kuwa, wiki iliyopita Saudi Arabia iliongoza Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Misri katika kukata uhusiano wao wa kidiplomasia na mahusiano yote ya majini na angani na Qatar zikiituhumu nchi hiyo kuwa inaunga mkono ugaidi na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo. Qatar imekanusha tuhuma hizo na kuzitaja kuwa zisizoa na msingi.

Aidha Saudia ilizitaka nchi waitifaki wake kukata uhusiano na Qatar na kwa msingi huo nchi kama vile Libya, Comoro, Mauritania, Maldives, Chad na Niger zimefuata kibubusa amri ya Saudi na kukata uhusiano na Qatar. Hatahivyo Somalia imesema haiwezi kukata uhusiano na Qatar nchi ambayo imekuwa ikiwasaidia Wasomali kwa muda mrefu. Msimamo huo wa Somalia unaonekana kuwakasirisha sana wakuu wa Saudi Arabia na UAE ambao mbali na  kuikatia Somalia misaada wakati nchi hiyo inakumbwa na njaa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, sasa wamewatimua wawakilishi wa Somalia katika mashindano ya Qur’ani Dubai.

Katika mashindano hayo ya Qur’ani ya Dubai, Mohamad Abdullah Ahmad Abdullah Ahmad ambaye alikuwa akiwakilisha Qatar hakuruhisiwa kushiriki katika mashindnao hayo ya Dubai. Wakuu wa UAE wanadai kuwa Qatar inaunga mkono ugaidi na kuingilia mambo ya ndani ya nchi zingine.

Hatua hiyo imekosolewa na wanaharakati wa Qur’ani wamesema masuala ya siasa hayapaswi kuingizwa katika mashindano ya Kitabu cha Allah ambacho kinahimiza umoja na mshikamano wa Waislamu.UAE yaingiza siasa mashindanoya Qur’ani, wawakilishi wa Qatar, Somalia watimuliwa

Mwakilishi wa Somalia katika mashindano hayo ya Dubai, Ismail Omar Mattar amesema alikuwa anatazamiwa kushika nafasi ya kwanza katika amshindano hayo. Amebainisha masikitiko yake kuwa ametimuliwa katika mashindano hayo tena kwa njia ya udhalilishaji. Inasemekana wakuu wa mashindano hayo ya Qur’ani Dubai walimpa mwakilishi wa Somalia muda wa dakika 10 kuondoka katika ukumbi wa mashindano baada ya kuwa walishamkaribisha mapema. Pamoja na kuwa Somalia imeshatangaza kutopendelea upande wowote katika mgogoro wa Qatar na nchi kadhaa za Kiarabu, UAE imemuita nyumbani balozi wake aliye Mogadishu, Somalia.

Wakati huo huo Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar, Sheikh Abdulrahman Al Thani amekosoa pia kimya na msimamo dhaifu ulioonyeshwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kuhusu mvutano uliojitokeza hivi karibuni na kueleza kuwa, katika mazingira kama haya taasisi za kieneo zinapasa kuwa na nguvu, hata hivyo akasema taasisi hizo mbili imma zimekaa kimya auzimeonyesha msimamo usio wa wazi nawenye kutia shaka.

3609272

captcha