Ayatullah Khamenei amemtaka Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
kuelekeza jitihada zake katika kutekeleza uadilifu, kuwatetea wale wote
walionyongeshwa na maskini, kutekeleza sheria za Kiislamu, kuimarisha
umoja na heshima ya taifa na kutilia maanani uwezo mkubwa wa nchi na
kuwa wazi katika kutukuza thamani na misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Halikadhalika katika sherehe hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran ametoa ripoti kuhusu namna uchaguzi wa 12 wa Rais ulivyofanyika hapa nchini.
Kwa mujibu wa kifungu cha 110 cha Katiba ya Iran, miongoni mwa majukumu na mamlaka ya Kiongozi Muadhamu ni kusaini na kupasisha dikrii ya Rais wa nchi baada ya kuchaguliwa na wananchi. Kipindi cha urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miaka minne na Rais huanza kutumikia wadhifa wake baada ya tarehe ya kuidhinishwa hati za utambulisho wake na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Hassan Rouhani kwa mara nyingine tena alichaguliwa kuwa Rais wa Iran katika duru ya 12 ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanyika Mei 19 mwaka huu kwa kupata kura zaidi ya milioni 23 au tarkibani asilimia 57 ya kura zilizopigwa.