"Nitalinda dini rasmi ya nchi hii, Utawala wa Jamhuri ya Kiislamu na Katiba ya Iran, na nitatumia nguvu na mamlaka yangu katika kutekeleza majukumu niliyopewa na kujisabilia kwa ajili ya kuhudumia wananchi, kustawisha nchi, kueneza dini na maadili, kuunga mkono haki na uadilifu, na kujiepusha na udikteta. Nitatetea uhuru na heshima za watu na haki za taifa zilizoainishwa na Katiba", amesema Rais Rouhani wakati anaapisha bungeni.
Baada ya kuapishwa rasmi, Rais Rouhani alitia saini hati ya kiapo
mbele ya Mkuu wa Idara ya Mahakama hapa nchini na wajumbe wa Baraza la
Kulinda Katiba.
Kwa mujibu wa kifungu cha 110 cha Katiba ya Iran, miongoni mwa majukumu na mamlaka ya Kiongozi Muadhamu ni kusaini na kupasisha dikrii ya Rais wa nchi baada ya kuchaguliwa na wananchi. Kipindi cha urais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miaka minne na Rais huanza kutumikia wadhifa wake baada ya tarehe ya kuidhinishwa hati za utambulisho wake na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Hassan Rouhani kwa mara nyingine tena alichaguliwa kuwa Rais wa Iran
katika duru ya 12 ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
uliofanyika Mei 19 mwaka huu kwa kupata kura zaidi ya milioni 23.