IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Misri kupewa jina la Sheikh Abdul Basit

15:50 - October 23, 2019
Habari ID: 3472184
TEHRAN (IQNA) – Wizara ya Wakfu nchini Misri imetangaza kuwa duru ijayo ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani nchini humo imepewa jina la Qari maarufu wa nchi hiyo, al marhum Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad.

Kwa mujibu wa taarifa, Wizara ya Wakfu Misri imetoa taarifa na kusema uamuzi huo unalenga kumuenzi Qari huyo mashuhuri.

Duru ya 27 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Misri imepengwa kufanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Cairo, mwezi Februari mwaka 2020.

Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad alikuwa miongoni mwa makarii na wasomaji mashuhuri wa kimataifa wa Qur'ani Tukufu na weledi wa masuala ya Qur'ani wanamtambua kuwa ndiye karii mkubwa zaidi wa Qur'ami kote duniani. Ustadh Abdus Samad alibuni na kuanzisha mbinu makhsusi ya kiraa ya Qur'ani.

Abdul Basit alizaliwa mwaka 1927 katika kijiji cha Almazaizah katika eneo la Armant kusini mwa Misri. Babu yake, Ustadh Abdul Samad, alikuwa mtu aliyesifika kwa kuwa na takwa na kumcha Mwenyezi Mungu na miongoni mwa mahafidhi wa Qur'ani na vilevile mtaalamu wa masuala ya Qur'ani.

Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad alikamilisha hifdhi ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 10 kijijini kwake kwa Ustadh Al Amir na akahitimu aina zote za kiraa ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 14.

Abdul Basit alipewa lakabu ya 'Koo ya Dhahabu' kutokana na kiraa yake ya kuvutia na alipendwa mno na wafuatiliaji wa masuala ya Qur'ani kwa kadiri kwamba hadi sasa anatambuliwa kuwa karii mashuhuri na anayepesndwa zaidi wa Qur'ani.

Alianza kujifunza Qur'ani Tukufu akiwa bado mtoto mdogo na alipewa tuzo ya kuhifadhi na kusoma Qur'ani akiwa na umri wa miaka 12. Kipindi fulani Sheikh Abdul Basit alitumia muda wake mwingi kusafiri katika nchi za Kiislamu na kuwahamasisha watu kusoma kitabu cha Mwenyezi Mungu.

Mwaka 1952 Sheikh Abdul Swamad alikwenda kuhiji Makka na kusoma Qur'ani katika Masjidul Haram na Masjidunnabi huko Madina. Vilevile alikwenda Palestina na kusoma Qur'ani huko Baitul Muqaddas na katika Haram ya Nabii Ibrahim AS

Qiraa ya Sheikh Abdul Basit Abdul Swamad iliwaathiri watu wengi na hata kuwavutia wasiokuwa Waislamu katika dini ya Kiislamu. Watu 6 waliingia katika dini ya Kiislamu baada ya kuathiriwa na kiraa yake mjini Los Angeles huko Marekani. Aidha inadokezwa kuwa nchini Uganda jumla ya watu 92 walisilimu katika majlisi ya kiraa ya msomaji huyo mashuhuri na watu wengine 72 pia walikubali dini tukufu ya Kiislamu katika majlisi nyingine baada ya kuvutiwa mno na usomaji wake.

Mwishoni mwa umri wake, Sheikh Abdul Basit alipatwa na maradhi ya kisukari na baadaye uvimbe wa ini. Alipelekwa London Uingereza kwa ajili ya matibabu baada ya kuzidiwa na maradhi na kurejeshwa Cairo wiki mbili baadaye. Inasemekana kwamba Ustadh Abdul Basit Abdus Samad alikuwa amehisi kwamba siku zake za kuishi duniani zinakaribia ukingoni na wakati wa kukutana na Mola Muumba ulikuwa unakaribia.

Qari huyo mashuhuri wa Misri aliaga dunia tarehe 30 Novemba mwaka 1988 katika mji mkuu wa Misri, Cairo.

Ustadh Abdul Basit ameacha kanda nyingi za Sauti ya qiraa yake ya Qur'ani Tukufu ambazo bado zinawavutia wengi wengi duniani.

3851893

captcha