IQNA

Katibu Mkuu wa UN asema bado ana hofu kuhusu hali ya Waislamu wa Myanmar

7:33 - November 05, 2019
Habari ID: 3472201
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema bado anaendelea kuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya Myanmar, ikiwemo katika jimbo la Rakhine kutokana na kukandamizwa Waislamu wa jamii ya Rohingya katika eneo hilo.

Guterres amesema hayo huko Bangkok, Thailand wakati akihutubia mkutano wa 10 wa ngazi ya juu kati ya Umoja wa Mataifa na jumuiya ya nchi za kusini-mashariki mwa Asia, ASEAN.

“Inasalia bila shaka kuwa ni wajibu wa Mynmar kushughulikia visababishi vya raia kukimbia jimboni Rakhine na kuhakikisha kuwa kuna mazingira salama kwa wakimbizi kurejea nyumbani kwa hiari, kwa utu na kwa uendelevu huko jimboni Rakhine, na hivyo vifanyike kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” amesema Katibu Mkuu.

 Ametaja mambo ya kuzingatia kuwa ni pamoja na taifa hilo kuwezesha kufanyika kwa mazungumzo na wakimbizi na kuweka mazingira ya kurejea kwa imani.

Halikadhalika kuridhia bila kuchelewa miradi ya matokeo ya haraka ya kuwezesha wakimbizi wanaorejea kuwa na njia za kujipatia kipato sambamba na miundombinu, huduma za msingi na za ulinzi na usalama, “na kuharakisha suluhu kwa wale ambao bado wamesalia kuwa wakimbizi wa ndani nchini humo.”

Katibu Mkuu amesema hatua zote hizo ni lazima zizingatie mapendekezo ya Kamisheni ya Ushauri kwa jimbo la Rakhine ambayo itahitaji kufuatilia kwa umakini.

Hata hivyo ametumia hotuba yake kukaribisha hatua za hivi karibuni za ASEAN kushauriana na Myanmar na amesihi juhudi hizo ziendelee.

Baada ya kuhutubia mkutano huo, Katibu Mkuu alikuwa na mkutano na waandishi wa habari ambapo aliulizwa swali kuhusu mustakabali wa wakimbizi wa Rohingya na juhudi za ASEAN katika kushughulikia suala hilo ambapo amesema kuwa, “alijulishwa kuwa ASEAN inashauriana kwa karibu zaidi na serikali ya Myanmar na kwamba kuna kikosi kazi maalum kimeundwa kufuatilia juhudi hizo.”

Hata hivyo amesema jambo muhimu zaidi ni kuweka mazingira ya kuwepo kwa maridhiaono ya dhati baina ya jamii.

“Katika jimbo la Rakhine kuna jamii ya Warohingya. Ni muhimu kuweka mazingira ya maridhiano ya kuwezesha kutokomezwa kwa kauli za chuki, kuwezesha kutoweka kwa kauli za chuki na wengine kukataliwa, na vikosi vya jeshi na polisi viwe chachu ya maridhiano na si visababishi vya mateso, ili hatimaye watu wajihisi wako salama kurejeah nyumbani na wanaerejea kwa utu na kwa hiari,” amesema Katibu Mkuu.

Agosti 25 mwaka 2017 Waislamu wapatao 740,000 wa jamii ya Rohingya walilazimika kuyahama makazi yao kwa umati katika jimbo lao la Rakhine na kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh walikojiunga na wenzao wengine laki mbili waliokuweko nchini humo, baada ya vikosi vya jeshi la Myanmar kuanzisha wimbi kubwa la hujuma na ukandamizaji dhidi ya Waislamu hao.

Aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein aliesema kuwa uhalifu unaofanywa na Mabudha kwa himaya ya serikali nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari.

3469796

captcha