IQNA

Kongamano la Kimataifa la 'Imam Khomeini na Ulimwengu wa Kisasa'

15:46 - June 03, 2021
Habari ID: 3473975
TEHRAN (IQNA)- Kongamano la Kimataifa la 'Imam Khomeini na Ulimwengu wa Kisasa" linafanyika leo katika Haram ya Imam Khomeini-Mwenyezi Mungu Amrehemu-Kusini mwa Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa kongamano hilo linafanyika Alhamisi hii kuanzia saa 11 hadi saa mbili usiku kwa mnasaba wa kukumbuka mwaka wa 32 wa kuaga dunia Imam Khomeini MA, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kongamano hilo limeandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Imam Khomeini (MA) na Mapinduzi ya Kiislamu, Shirika la Habari la Qur'ani la Kimataifa, Taasisi ya Kukusanya na Kuchapisha Fikra za Imam Khomeini (MA) na Idara ya Maadhimisho ya Kuaga Dunia Imam Khomeini (MA).

Kati ya wanaohutubu katika kikao hicho ni Hujjatul Islam Ali Kamsari ambaye anasimamia Taasisi ya Kukusanya na Kuchapisha Fikra za Imam Khomeini (MA) huku hotuba kuu ikitolewa na Ayatullah Sayyid Hassan Khomeini.

Wazungumzaji wengine katika kongamano hilo ni Mostafa Rostami, mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika vyuo vikuu, Shafiq Dayoub Balozi wa Syria nchini Iran na Nasser Abu Sharif, mwakilishi wa Harakati ya Jihad Islami nchini Iran.

Balozi wa Palestina nchini Iran Salah al-Zawawi na Naibu Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem wanatuma ujumbe kwa njia ya video.

Juni 3 1989, yaani miaka 32   iliyopita, Imam Ruhullah Musawi Khomeini (MA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87. Baada ya kutangazwa habari ya kufariki kwake dunia, ilimwengu wa Kiislamu uligubikwa na wingu la simanzi na huzuni. Imam Khomeini alizaliwa tarehe 24 Septemba mwaka 1902 huko katika mji wa Khomein katikati mwa Iran. Alianza harakati zake za kisiasa sambamba na shughuli zake za kielimu na kiutamaduni.

Kutokana na shughuli zake za kisiasa zilizokuwa zikiukera sana utawala wa kidhalimu wa mfalme Shah, utawala huo ulimbaidisha Imam katika nchi za Uturuki na Iraq. Katika kipindi cha miaka 13 akiwa uhamishoni huko Iraq, Imam (MA) alilea na kuwafunza wanafunzi wengi na wakati huohuo kufichua maovu yaliyokuwa yakifanywa na utawala wa Shah kwa ushirikiano wa karibu na Marekani.

Baada ya kupamba moto mapambano na harakati za Kiislamu zilizokuwa zikiongozwa na Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah, hatimaye Imam alilazimika kutoka nchini Iraq na kuhamia Ufaransa, hadi Mapinduzi ya Kiislamu yalipopata ushindi hapa nchini hapo mwaka 1979. Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu wote duniani kwa mnasaba huu mchungu wa kukumbuka siku aliyoaga dunia Imam Khomeini (MA), mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran.

3975041

Kishikizo: iran imam khomeini
captcha