IQNA

Ansarullah

Al Houthii: Israel inajipenyeza Asia Magharibi kupitia matanao na tawala za Kiarabu

21:13 - May 20, 2022
Habari ID: 3475269
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameashiria mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu na kusema mapatano kama hayo yatatoa mwanya kwa utawala wa Tel Aviv kujipenyeza zaidi Asia Magharibi.

Akihutubia ujumbe wa viongozi wa kikabila kutoka mkoa wa magharibi mwa Yemen wa Ibb Alhamisi jioni, Kiongozi wa Ansarullah Sayyid Abdul-Malik Badruldeen al-Houthi amesema nchi za Kiarabu ambazo zimeanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ndio ambazo zinaonyesha uadui na kutekeleza hujuma ya kijeshi dhidi ya Yemen. Amesema maadui wanalenga kuvuruga umoja wa Yemen lakini Wayemen watendelea katika mkono wao wa uhuru na kujitegemea na hawatawaruhusu wageni waingilie mambo yao ya ndani.

Kwingineko katika hotuba yake, Kiongozi wa harakati ya wananchi ya Ansarullah ya Yemen amesema Marekani, ikishirikiana na magaidi wakufurishaji ambao ni waitifaki wake, inajenga vituo kadhaa vya kijeshi katika mikoa ya mashariki mwa nchi hiyo ya Hadhramaut na al-Mahrah na halikadhalika mji wa Aden na pwani ya Bahari ya Sham.

Al-Houthi ameashiria ujenzi wa vituo hivyo vya kijeshi vya Marekani nchini humo na kusema Wayemen hawatakubali kupokea amri kutoka Washington. Aidha ametahadharisha kuwa maadui wanafanya juu chini  kuibua mifarakano na migawanyiko baina ya watu wa Yemen.

Al Houthi amesema maadui sasa wanatumia fursa iliyojitokeza ya usiitishwaji vita unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa kujitayarisha kwa awami nyingine ya vita kwa sababu walifeli katika miaka iliyopita.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ikishirikiana na UAE na kwa himaya ya Mareakni na utawala haramu wa Israel na madola mengine ya Magharibi ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Vita vilivyoanzishwa  na Saudi Arabia na washirika wake dhidi ya Yemen na kuendelea hadi sasa vimeshapelekea mamia ya maelfu ya watu wasio na hatia kupoteza maisha, mbali na kuwaacha mamilioni wakiwa hawana pa kuishi. Aidha vita hivyo vimesababisha matatizo mengi ya ukosefu wa chakula, matibabu na elimu kwa watu wa Yemen.

Katika kulipiza kisasi jinai hizo, Jeshi la Yemen hutekeleza mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maeneo ya kistratijia ya Saudi Arabia na UAE.

 

4058246

captcha