IQNA

Qur'ani inasema nini / 7

Mtazamo wa Qur'ani kuhusu wengine kuwatawala Waislamu

17:04 - June 10, 2022
Habari ID: 3475360
TEHRAN (IQNA) – Moja ya matatizo makubwa wanayokumbana nao Waislamu ni kutawaliwa na wasio Waislamu au makafiri katika maeneo mbali mbali duniani. Nini mtazamo wa Qur'ani juu ya hili?

Uislamu unawaheshimu wafuasi wa dini nyingine lakini unasisitiza kwamba mahusiano ya kirafiki ya Waislamu na wafuasi wa dini nyingine yanapaswa kuwa katika misingi ya imani na Taqwa (kumcha Mungu).

Kuna aya nyingi ndani ya Qur'ani Tukufu ambazo zinawakataza Waislamu kukubali kudhibitiwa au kuwa duni mbele ya wale wanaofuata imani nyingine.

Mwenyezi Mungu amewaamrisha Waislamu kudumisha heshima na uhuru wao katika nyanja zote za maisha, zikiwemo za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa, na kutotafuta heshima na uhuru kwa kutegemea urafiki na maadui wa Uislamu. Waislamu wametakiwa kumtegemea Mwenyezi Mungu ambaye ndiye chimbuko la heshima zote katika nyanja zote.

Moja ya aya za Qur'ani zinazozungumzia suala hili ni Aya ya 141 ya Sura An-Nisa:  "Wale ambao wanakungojeeni, mkipata ushindi unao toka kwa Mwenyezi Mungu wao husema: Si tulikuwa pamoja nanyi vile? Na ikiwa ni sehemu ya makafiri kushinda wao huwaambia: Hatukuwa ni waweza wa kukushindeni, nasi tukakukingeni na hawa Waumini? Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama, wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini."

Inajulikana kama Aya ya "Nafy Sabil" (kukataa mamlaka ya wasioamini juu ya waumini).

Nafy Sabil ni kanuni ya Kiislamu inayokataza umma wa Kiislamu kudhibitiwa  na wasioamini katika sekta yoyote ile iwe ni ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni, kiuchumi na kijeshi.

Mafaqihi (wataalamu wa sheria za Kiislamu) wanarejea kwenye maneno “Mwenyezi Mungu hatawapa njia…” ili kuja na kanuni hii ya Waislamu kutoruhusu wasiokuwa Waislamu kuwa na mamlaka katika mfumo wao wa maisha.

Pamoja na hayo, hakuna shaka kuwa, ni sawa kwa Waislamu kuwa na mafungamano na wafuasi wa imani nyingine ili kujifunza kutoka kwao na kuwa na mabadilishano ya kiutamaduni na kiuchumi ikiwa hayasababishi wasiokuwa Waislamu kuwatawala katika masuala yao ya kimaisha. Kwa hakika kuna Hadithi kutoka kwa Mtukufu Muhammad SAW isemayo: “Tafuta elimu hata kama itabidi uende China”. Kutaja China hapa kunaashiria umbali wa mbali na tofauti za kitamaduni.

Katika Tafsiri yake ya Nur ya Qur'ani Tukufu, Sheikh Muhsin Qara’ati anasema kuhusu aya hii kwamba Quran inautaja ushindi wa Waislamu kuwa ni Fat’h na ushindi wa makafiri kama Naseeb. Inaweza kuashiria kwamba faida za makafiri ni za muda ilhali ushindi wa mwisho ule wa kweli na wa haki ambao ni wa Waislamu.

Habari zinazohusiana
captcha