IQNA

Arbaeen ya Imam Hussein AS

Maonyesho ya Qur'ani yazinduliwa kwenye njia ya wafanyaziara ya Arbaeen

15:49 - September 10, 2022
Habari ID: 3475761
TEHRAN (IQNA) - Maonyesho ya Qur'ani Tukufu yamewekwa kwenye barabara kati ya miji mitukufu ya Najaf na Karbala nchini Iraq wakati wa msimu wa Arbaeen.

Taasisi ya Qur'ani ya Najaf yenye mafungamano na Kituo cha Dar-ul-Quran cha Mfawidhi wa Haram Takatifu ya Hazrat Abbas (AS) imeandaa maonyesho hayo.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo Muhnad al-Miyali amesema mabanda 7 katika maonyesho hayo yanaonesha shughuli zake za Qur'ani, utafiti, vyombo vya habari na nyinginezo ambazo zinalenga kuendeleza mafundisho ya Qur'ani.

Amesema kando ya maonyesho hayo yatakayodumu kwa muda wa siku kumi, kutakuwa na vikao vya qiraa ya  Qur'ani Tukufu na shughuli zingine kadhaa zenye kuwalenga wafanyaziara.

Taasisi hiyo pia imeweka kituo maalumu  kwa ajili ya kutoa mafunzo kuhusu usomaji wa Sura za Qur'ani ambazo husomwa sana wakati wa sala tano za  kila siku sambamba na kujibu maswali ya wafanyaziara katika uwanja wa Qur'ani, dini, Fiqh n.k.

Mashindano kuhusu mafanikio ya wanazuoni wa Kiislamu katika nyuga za Qur'ani, pamoja na mashindano ya uchoraji kwa watoto ni miongoni mwa programu nyingine kwa ajili ya mahujaji, aliendelea kusema.

Maadhimisho ya Arbaeen (Arubaini) ni mojawapo ya mikusanyiko mikubwa ya kidini duniani.

Siku hii huadhimishwa  siku ya 40 baada ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein (AS) tarehe 10 Muharram katika Siku ya Ashura.

Kila mwaka, wafanyaziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri njia ndefu kwa miguu hadi Karbala, ambako ndiko kunako haram takatifu la Imam Hussein (AS).

Siku ya Arbaeen mwaka huu inasadifiana na Septemba 17 mwaka huu.

Wafanyaziara, hasa kutoka Iraq na Iran, husafiri njia ndefu kwa miguu hadi mji mtakatifu wa Karbala.

captcha