IQNA

Wahusika wa Karbala /1

Wale waliokuwa na udhuru wa kutokwenda Karbala

16:44 - September 10, 2022
Habari ID: 3475763
TEHRAN (IQNA) – Tukio la Karbala lina mafunzo mengi kwa wanadamu. Katika Vita vya Karbala vya mwaka 61 Hijria Qamaria au 680 Miladia, pande za ukweli zilikabili upande wa batili na uongo.

Miaka 1383 iliyopita tarehe 10 Muharram katika siku ya Ashura, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala katika Iraq ya leo.

Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

Katika mapambano hayo, misimamo ya watu ilibainika kulingana na hatua walizochukua.

Pia kulikuwa na watu ambao hawakuhudhuria vita hivyo na kushindwa kupigana bega kwa bega na Imam Hussein (AS). Baadhi yao walikuwa na udhuru kwa hilo. Wanaitwa Ma’dhureen (wale waliokuwa na udhuru).

Mmoja wao alikuwa Mukhtar ambaye alimkaribisha Muslim bin Aqeel huko Kufa. Hakuweza kupigana katika Vita vya Karbala kwa sababu alikuwa amefungwa na Ibn Ziyad.

Baadhi ya wafuasi wa Imam Hussein (AS) hawakuweza kufika Karbala kwa sababu njia ilikuwa imefungwa. Wengine hawakupokea habari kwa wakati.

Kulikuwa na baadhi ya watu wa Bani Hashim (ukoo wa kabila la Quraysh ambalo Mtume Muhammad (SAW) alitoka) ambao mtu angetarajia kuwepo Karbala lakini hawakufika kwa mfano Abdullah ibn Abbas, ambaye alikuwa miongoni mwa masahaba wa Imam Ali (AS), na Abdullah ibn Ja'far, mume wa Bibi Zeynab (SA).

Kuhusu Abdullah ibn Abbas, imesemekana kwamba alikuwa kipofu na hakuweza kushiriki katika vita. Lakini kwa ujumla, inaonekana kwamba yeye na Abdullah ibn Ja’far walikosa busara au umaizi unaohitajika.

Ama kuhusu Muḥammad ibn al-Ḥanafīyya ,  mwana wa tatu wa Imam Ali AS inaonekana kwamba alijiona kuwa anastahili zaidi kuliko Imam Hussein (AS) kwa uongozi na asingekubali mawazo na harakati za Imam Hussein (AS). Hili liko wazi kutokana na nasaha zake kwa Imam Hussein (AS). Bila shaka wengine wanasema alikuwa mgonjwa na ndiyo maana hakufuatana na Imam (AS) lakini haionekani kuwa hivyo kwa sababu hata hakumtuma mwanawe kumuunga mkono Imam Hussein (AS).

Kumay ibn Ziyad Al-Assadi na Ghanbar ni miongoni mwa watu wengine ambao hawakwenda Karbala. Walikuwa watiifu wa Ahl-ul-Bayt (AS) na waliuawa kishahidi na watawala wa Bani Umayya baada ya Vita vya Karbala lakini historia inakaa kimya kwa nini hawakuwapo hapo Karbala.

Kulikuwa na mwanamke aliyeitwa Mariya binti Saad ambaye hakufika Karbala lakini alikuwa na jukumu muhimu. Nyumba yake huko Basra ilikuwa ni mahali ambapo waja wa Ahl-ul-Bayt (AS) walikusanyika. Wakati mjumbe wa Imam Hussein (AS) alipofika Basra na kuwapa ujumbe wa Imam (AS), Mariya alikusanya idadi ya watu kwenda Karbala na kuungana na Imam Hussein (AS). Walikuwa wakielekea Karbala na kabla ya kufika walisikia habari za kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na masahaba zake.

captcha