IQNA

Jamii ya kimataifa yalaani hujuma dhidi ya msikiti wa Mashia Saudi Arabia

15:04 - May 23, 2015
Habari ID: 3306740
Jamii ya kimataifa inaendelea kulaani vikali shambulio la kigaidi dhidi ya msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani vikali mashambulizi  hayo ya  Ijumaa  yalioyolenga msikiti wa Kishia katika mji wa al-Quidaih katika eneo la Qatif Mashariki la Ufalme wa Saudia.

Waislamu 21 wameuawa shahidi na 100 wengine kujeruhiwa katika shambulio la jana la kigaidi lililotokea wakati Waislamu wakiwa wamejaa katika msikiti  wa Imam Ali AS kusali Sala ya Ijumaa. Kundi la kitakfiri la Daesh limetangaza kuhusika na shambulio hilo la kigaidi.

Taarifa ya msemaji wa Katibu Mkuu imemkariri Ban akisisitiza kwamba mashambulizi kama hayo ya maeneo ya ibada hayakubaliki na yana lengo la kuzua mzozo wa kidini huku ikiongeza kwamba anatarajia kwamba sheria itachukua mkondo wake.

Ammar al Hakim, Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq ametaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika wa shambulio hilo la kigaidi lililofanyika katika msikiti wa Imam Ali AS huko mashariki mwa Saudi Arabia.

Jopo la Maulamaa Saudi Arabia pia wamelaani hujuma hiyo na kudai kuwa imetekelezwa na vibaraka wa kigeni. Mufti wa Misri amesema waliotekeleza hujuma hiyo wanalenga kuzusha hitilafu za kimadhehebu. Serikali za Qatar na Bahrain pia zimelaani hujuma hiyo na kutangaza kuwa tayari kuisaidia Saudi Arabia kupambana na ugaidi.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon sambamba na kulaani jinai hiyo imesema utawala wa Saudi Arabia ndio unaobeba dhima ya hujuma ya kigaidi dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia.../mh

3306420

captcha