IQNA

Tunisia yafunga misikiti 80 baada ya hujuma ya kigaidi

5:09 - June 28, 2015
Habari ID: 3320222
Serikali ya Tunisia imeamua kufunga misikiti 80 inayoendeshwa nje ya udhibiti wake, siku moja baada ya kutokea shambulio la kigaidi na kupelekea makumi ya watu kuuawa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Waziri Mkuu wa Tunisia Habib al Essid ametangaza habari hiyo Jumamosi na kusema kuwa, wananchi wa Tunisia wanapaswa kuwa kitu kimoja na kuisaidia serikali katika kupambana na makundi ya kigaidi.
Amesema, hakuna msikiti wowote utakaoruhusiwa kujiendesha nchini Tunisia bila ya serikali kujua unajiendesha vipi.
Hatua hiyo imechukuliwa baada ya mtu mmoja mwenye silaha kufanya mauaji ya watu 38 wengi wao wakiwa ni watalii, katika mji wa Sousse, kaskazini mwa Tunisia jana Ijumaa.
Vikosi vya usalama vya nchi hiyo vilimpiga risasi na kumuua mmoja wa washambuliaji wawili, huku mwingine akikimbia na hivi sasa anasakwa.
Kundi la kigaidi la Daesh au ISIS limetangaza kuhusika na shambulio hilo. Daesh inafanya jinai pia katika maeneo mengine duniani hususan Iraq na Syria.
Jana Ijumaa pia, kundi la kigaidi la Daesh lilifanya mauaji ya Waislamu zaidi ya 27 wa Kishia wakati Waislamu hao walipokuwa kwenye sala ya Ijumaa nchini Kuwait.
Jana hiyo hiyo, mtu mmoja mwenye uhusiano na kundi la kigaidi la Daesh aligongesha gari yake na kiwanda cha gesi katika eneo la Isère karibu na Grenoble, huko kusini mashariki mwa Ufaransa na kusababisha mripuko uliojeruhiwa watu wawili.
Vile vile alimkata kichwa mwajiri wake wa zamani na kutundika kichwa chake kwenye geti la kiwanda hicho pamoja na bendera ya genge la kigaidi la Daesh.../mh

3319997

captcha