IQNA

OIC yaalani hujuma za kigaidi ya Paris

6:12 - November 16, 2015
Habari ID: 3452963
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani vikali mashambulizi ya kigaidi ya juzi huko Paris mji mkuu wa Ufaransa.

Iyad Madani, Katibu Mkuu wa OIC amelaani mashambulizi ya kigaidi ya juzi Ijumaa usiku huko Paris yaliyoua watu wasio na hatia wasiopungua 130 na kutoa mkono wa pole kwa serikali, wananchi wa Ufaransa na familia za wahanga wa mauaji hayo. Iyad Madani amesema kuwa, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu siku zote inasisitiza juu ya msimamo wake thabiti katika kulaani aina zote za ugaidi na kuuangamiza kwa mujibu wa sheria na misingi mikuu ya dini ya Uislamu. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OIC amezitaka serikali zote duniani, taasisi za kimataifa na jumuiya za kiraia kuungana na kuwa kitu kimoja katika mapambano dhidi ya ugaidi, ambao ni adui nambari moja wa wanadamu kote duniani. Watu wasiopungua 130 waliuliwa na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyoanza kutekelezwa juzi usiku huko Paris mji mkuu wa Ufaransa na kuendelea hadi alfajiri. Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuhusika na mashambulio hayo ya kigaidi ya Paris.

3447939

captcha