IQNA

Mamilioni ya Waafrika, Wayemen wanakabiliwa na baa la njaa

18:25 - February 23, 2017
Habari ID: 3470866
IQNA: Umoja wa Mataifa umeonya kuwa baa la njaa limeenea katika nchi kadhaa za Afrika na Yemen ambapo mamilioni ya watu wakiwa katika hatari ya kupoteza maisha.

Katika taarifa siku ya Jumanne, mratibu wa masuala ya haki za binadamu Yemen Jamie McGoldrick amesema Wayemn milioni saba hawajui mlo wao wa utatoka wapi. Amekadiria kuwa Wayemen milioni 17 hawawezi kujimudu kupata milo mitatu kwa siku na hivyo wengi wanalazimika kupata mlo moja. Yemen imekuwa ikabiliwa na hujuma haramu ya kijeshi ya Saudi Arabia kwa muda wa miaka miwili sasa jambo ambalo limeitumbukiza nchi hiyo katika matatizo mengi sana.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema baa la njaa limeenea katika nchi kadhaa za Afrika na Yemen huku akisema hali ya Sudan Kusini ni mbaya sana

Akizungumza Jumatano katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari ukimjumuisha mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo UNDP Helen Clark, mratibu wa masuala ya binadamu wa Umoja wa Mataifa Stephen O'Brien na wadau wengine wakiwemo WFP, FAO na UNICEF amesema kikao hicho kimeitishwa kuufahamisha ulimwengu hali halisi ya njaa.

Guterres ameonya kwamba hali ni mbaya na dunia isipoziba ufa basi italazimika kujenga ukuta na kuongeza kuwa: "Leo hii watu zaidi ya milioni 20 Sudan Kusini , Somalia, Yemen , na Kaskazini Mashariki mwa Nigeria wanakabiliwa na njaa na hawana uhakika wa chakula".

Amesema endapo hatua hazitochukuliwa hivi sasa basi muda si mrefu hali hii itayakumba pia maeneo na nchi zingine.

Guterres ameonya kuwa moja ya vikwazo vikubwa ni fedha za ufadhili na kuongeza kuwa operesheni za kibinadamu katika nchi husika kwa muda wa miaka minne zinahitaji zaidi ya dola bilioni 5.6.

/3462271

captcha