IQNA

Muharram 1445

Taifa la Iran katika maombolezo ya Siku ya Tasua

11:30 - July 27, 2023
Habari ID: 3477347
TEHRAN (IQNA)- Waislamu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maeneo mengine ya dunia leo tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram wameshiriki katika vikao, majlisi na shughuli za maombolezo ya Tasua.

Katika shughuli hiyo ya Tasua ya kukumbuka misiba na masaibu yaliyomfika mjukuu wa Mtume wetu Muhammad (SAW0, Imam Hussein bin Ali (AS), ndugu na mswahaba zake waaminifu huko Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria, waumini waliokuwa wamevaa nguo nyeusi kama ishara ya huzuni na  maombolezo wamemkumbuka Abul Fadhl Abbas bin Ali, ndugu yake Imam Hussein AS ambaye ndiye aliyekuwa mbeba bendera na kamanda wa jeshi la mtukufu huyo katika mapambano ya siku ya Ashura.

Katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Tehran,majlisi za maombolezo na kuwakumbuka mashujaa wa Karbala hususan Abul Fadhl zimefanyika katika maeneo mbalimbali.

Katika siku ya 9 ya mwezi Muharram mahatibu na wazungumzaji humkumbuka zaidi Abul Fadhl Abbas ambaye alionesha ushujaa, wa hali ya juu katika mapambano ya Karbala na kuwakumbusha watu ushujaa usio na kifani wa baba yake, Ali bin Abi Twalib (AS).

Abul Fadhl al Abbas aliuawa shahidi siku ya tarehe kumi Muharram baada ya kukatwa mikono miwili na maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad SAW ambao kinara wao alikuwa ni Yazid bin Muawiyah.

Waumini 72 waliokuweko Karbala wote waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram katika siku ya Ashura wakiwa pamoja na kiongozi wao, Imam Hussein bin Ali AS katika mapambano ya haki dhidi ya dhulma na uonevu mapambano ambayo damu ya mashahidi hao ilizishinda panga za maadui.  

Mafunzo ya harakati ya Imam Husein (AS) yana historia na jiografia pana  na kamwe haiwezi kuwekewa mipaka. 

Karne nyingi zimepita tangu tukio la Karbala na kuuawa shahidi Imam Hussein (AS) na masahaba zake waaminifu,na sio tu umuhimu na hadhi ya tukio hili haijapungua, bali kadiri muda unavyosonga mbele, ujumbe wa Ashura unazidi kuwa mpana zaidi.

captcha