IQNA

Kongamano la kupambana na matakfiri lamalizika Cairo

19:04 - December 05, 2014
Habari ID: 2615265
Kongamano la Kimataifa la Kupambana na Ugaidi na Uchupaji Mipaka lililokuwa likifanyika katika taasisi ya al Azhar nchini Misri limesisitiza katika taarifa yake ya mwisho kuwa, makundi ya kitakfiri na yenye misimamo mikali hayana uhusiano wowote na Uislamu.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hatua ya kuwashambulia wafuasi wa dini nyingine na kuwalazimisha kuzihama nyumba zao, ni kinyume na misingi ya dini na ni jinai.Taarifa ya mwisho ya Kongamano la Kimataifa la Kupambana na Ugaidi na Uchupaji Mipaka lililofanyika huko Misri pia imewataka maulamaa wa dini kuwaelimisha vijana kuhusu dini na kuwaongoa vijana waliotumbukia katika upotofu.


Mkutano huo wa al Azhar umezitaka pia nchi za Kiarabu na Kiislamu kutekeleza majukumu yao ili kuzima moto wa mivutano ya kidini. Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesisitiza kuwa, katika Uislamu Jihadi ni kwa ajili ya kujihami tu na kukabiliana na uchokozi. Washiriki wa Kongamano la Kimataifa la Kupambana na Ugaidi na Misimamo Mikali lililofanyika nchini Misri wamelaani pia chokochoko za utawala wa Kizayuni wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo khususan huko Baitul Muqaddas na kusisitiza kuwa wanataka kuhitimishwa jinai za maghasibu wa Kizayuni dhidi ya matukufu ya Kiislamu ya Palestina na kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai wahusika wote wa hujuma hizo.

Kongamano la Kimataifa la Kupambana na Misimamo Mikali ya Kidin limefanyika katika taasisi ya al Azhar ya Misri kwa kuhudhuriwa na wanafikra 700 wa dini na madhehebu mbalimbali kutoka nchi 120 duniani.Akizungumza  katika ufunguzi wa kongamano hilo Sheikh Ahmed al Tayeb, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Al Azhar alilaani vikali 'jinai za kinyama' zinazofanywa na kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq na Syria. Mwanazuoni huyo wa ngazi za juu wa Kisuni amesema magaidi wa Kitakfiri wanaeneza taswira potofu kuhusu Uislamu duniani.../mh

2615171

captcha