IQNA

Wanawake Waislamu Marekani wajifunze kujihami

13:15 - March 14, 2016
Habari ID: 3470195
Wanawake Waislamu nchini Marekani wametakiwa kujifunza mbinu za kujilinda na kujihami wanaposhambuliwa kutokana na kuongezeka chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu nchini humo.
Wito huo umetolewa na Baraza la Mahusiano la Waislamu nchini Marekani ,CAIR, kupitia msemaji wake Ibrahim Hooper ambaye amebainisha umuhimu wa wanawake wa Kiislamu nchini humo kujifunza namna ya kujihami kimwili wanapohujumiwa na maadui wa Uislamu.
Hooper amesema hujuma dhidi ya Waislamu nchini Marekani zimeongezeka mara tatu katika kipindi cha miezi michache iliyopita na kwamba asilimia 80 ya hujuma hizo huwa dhidi ya wanawake wa Kiislamu.

Msemaji wa Baraza la Mahusiano la Waislamu nchini Marekani amesema chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani zimekithiri mno tangu baada ya shambulizi la kigaidi la Paris nchini Ufaransa Novemba mwaka jana, na hujuma ya makumi ya watu kuuawa kwa kufyatuliwa risasi katika mji wa San Bernardio jimboni California nchini Marekani Disemba mwaka huo huo. Hooper amesema chuki hizo ziliongezeka baada ya Donald Trump, Mgombea wa kiti cha rais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican kutoa pendekezo la kuzuiwa Waislamu kuingia nchini humo eti kwa lengo la kupambana na ugaidi.

Wakati huo huo Rana Abdulhamid, mtaalamu wa Karate wa daraja ya Ukanda Mweusi ameanzisha kampeni ya kuwapa mafunzo ya kujihami wanawake Waislamu wa Marekani. Mwanamke huyo wa Kiislamu akishirikiana na kundi lake wanatoa mafunzo ya kujihami kwa wanawake Waislamu katika mji wa New York ili waweze kujilinda endapo watashambuliwa na mtu kwa sababu ya chuki za kidini.

Akizungumzia mpango huo, Rana Abdulhamid amesema wanawake Waislamu, sasa wana nyenzo zaidi za kujihami endapo watakabiliwa na vitendo vya kikatili, ikiwemo kukwepa kwa kukimbia au kutumia umahiri wa kupambana ili kujihami.

3483080
captcha