IQNA

Waislamu Marekani wamlaani Cruz kwa matamshi yake yaliyojaa chuki

16:52 - March 24, 2016
Habari ID: 3470212
Waislamu nchini Marekani Baraza wamemkosoa mgombea uteuzi wa kiti cha rais katika chama Republican Ted Cruz kufuatia matamshi yake ya kutaka Waislamu wafanyiwe msako mkali.

Cruz amependekeza kuazishwa msako mkali dhidi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu eti kwa shabaha ya kuwazuia ‘wasiingie kwenye kundi la wenye misimamo iliyofurutu ada’.

Cruz aliyasema hayo masaa machache baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu wa Ubelgiji Brussels siku ya Jumanne ambapo watu 34 walipoteza maisha.

Matamshi ambayo yamewaghadhabisha viongozi wa kidini na watetezi wa haki za binadamu nchini Marekani. Kadhalika mwanasiasa huyo ambaye anaonekana kufuata nyayo za mgombea mwenzake wa chama cha Republican, Donald Trump, amesema kuna haja ya kuimarisha usalama katika mipaka ya nchi hiyo ili kuzia wale aliyowataja kuwa watu wenye misimamo mikali.

Baraza la Mahusiano ya Kiislamu la Marekani limeelezea kusikitishwa kwake na matamshi ya chuki ya mwanasiasa huyo wa chama Republican na kusema kuwa, kauli za aina hii hazitakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuzidisha ubaguzi wa kidini na chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu duniani. Nihad Awad, Mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo amesema matamshi ya Cruz sawa na yale yanayotolewa na Trump, yanakanyaga uhuru wa kuabudu na kuhatarisha maisha ya jamii ya Waislamu nchini Marekani.

Viongozi wa Kiislamu nchini Marekani wamesema kuwa maneno ya chuki dhidi ya Uislamu yanayotolewa na wanasiasa wa chama cha Republican, ndiyo sababu ya kuongezeka hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini humo. Taarifa iliyotolewa hivi karibuni na viongozi wa jumuiya za Waislamu nchini Marekani mjini Washington ilimtaka Trump, kuwaomba radhi Waislamu kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni yaliyojaa chuki dhidi yao.

3459389

captcha