IQNA

Waislamu Marekani wahofia chuki dhidi ya Uislamu

15:09 - March 26, 2016
Habari ID: 3470215
Waislamu nchini Marekani wanakabiliana na wimbi jipya la chuki dhidi ya Uislamu au Islamophobia hata baada ya kuwa wamelaani vikali hujuma ya kigaidi mjini Brussels, Ubelgiji Jumanne hii.

Baada ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh kudai kuhusika na hujuma za Brussels, viongozi wa Kiislamu huko California, New York, Ohio na maeneo mengine ya Marekani walilaani hujuma hizo na kuonya kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Katika mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na kauli za wanasiasa wanaowania urais kunasikika matamshi ya chuki dhidi ya Waislamu.

Nabil Shaikh, kiongozi wa Jumuiya ya Wanachuo Waislamu katika Chuo Kikuu cha Princeton anasema baada ya kila hujuma ya kigaidi, huwa ni wakati mgumu sana kwa wanafunzi Waislamu.

Kwa mujibu wa Idara ya Masuala ya Umma ya Waislamu MPAC, mjini Washington DC, jamii za Waislamu kote Amerika Kaskazini zinajitayarisha kukabiliwa na hujuma za wanaopinga Uislamu na Waislamu.

Mgombea wa kiti cha rais kupitia chama cha Republican Ted Cruz amependekeza kuazishwa msako mkali dhidi ya wafuasi wa dini ya Kiislamu eti kwa shabaha ya kuwazuia ‘wasiingie kwenye kundi la wenye misimamo iliyofurutu ada’.

Cruz ameyasema hayo saa chache baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu wa Ubelgiji Brussels, matamshi ambayo yamewaghadhabisha viongozi wa kidini na watetezi wa haki za binadamu nchini Marekani. Kadhalika mwanasiasa huyo ambaye anaonekana kufuata nyayo za mgombea mwenzake wa chama cha Republican, Donald Trump, amesema kuna haja ya kuimarisha usalama katika mipaka ya nchi hiyo ili kuzia wale aliyowataja kuwa watu wenye misimamo mikali.

3484532


captcha