IQNA

Wanawake Waislamu Malawi Ruhsa Kuvaa Hijabu katika Picha za Leseni

14:22 - May 31, 2017
Habari ID: 3471002
TEHRAN (IQNA)-Wanawake Waislamu nchini Malawi sasa wanaweza kupigwa picha za leseni ya kuendesha gari wakiwa wamevaa vazi la staha la Hijabu.

Uamuzi huo umechukuliwa kufuatia mapatano baina ya Idara ya Trafiki na Huduma za Usalama Barabarani (DRTSS) na Jumuiya ya Waislamu Malawi (MAM).

Kulikuwa na mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kufuatia sharti la DTRSS la kuwataka wanawake Waislamu wavue Hijabu wakati wa kupigwa picha kwa ajili ya leseni.

Kwa mujibu wa Sheria za Trafiki Malawi za Mwaka 2000, wenye kuchukua leseni ya kuendesha gari wanapaswa kupigwa pasina kuvaa chochote kichwani.

Sheria hiyo imekuwa ni ya kidhalimu kwa wanawake Waislamu ambao kwa mujiibu wa mafundisho ya Uisalmu wanapaswa kuvaa Hijabu kamili inayojumuisha kufunika kichwa.

Baadhi ya wanawake Waislamu Malawi walikuwa wameshaamua kutochukua leseni za kuendesha gari kutokana na sharti hilo la kuwalazimu kuvua Hijabu jambo ambalo linakiuka mafundisho ya Kiislamu.

DTRSS imesema uamuzi wa kuwarushusu wanawake Waislamu wavae Hijabu katika picha za leseni umefikiwa baada ya mazungumzo yenye mafanikio na Jumuiya ya Waislamu Malawi.

Kwa mujibu wa mapatano hayo, wanawake hawatatakiwa kuvua Hijabu kikamilifu lakini watatakiwa kuhakikisha kuwa uso unaonekana kwa njia ya wazi.

3462997

captcha