IQNA

Mahakama Nigeria yapinga lalamiko la Sheikh Ibrahim Zakzaky

8:54 - July 08, 2017
Habari ID: 3471056
TEHRAN (IQNA)- Mahakama katika mji wa Kaduna nchini Nigeria imetupilia mbali lalamiko lililowasilishwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu kuhusu hatua ya jeshi la nchi hiyo kukiuka haki za binadamu.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Sheikh Ibrahim Zakzaky aliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu ya Shirikisho mjini Kaduna alipwe fidia ya naira bilioni mbili sawa na dola milioni 5.6 kama fidia ya madhara yaliyosababishwa kufuatia ghasia zilizosababishwa na wanajeshi wa serikali mwaka 2015 na mauaji ya mamia ya wafuasi wake katika mji wa Zaria kaskazini mwa Nigeria. Sheikh Zakzaky mwenyewe alijeruhiwa na amekuwa akishikiliwa na vyombo vya usalama katika eneo lisilojulikana tangu wakati huo. Watoto watatu wa kiongozi huyo pia waliuawa na makazi yake yaliharibiwa.

Dari Bayero, wakili anayelitetea jeshi la Nigeria katika kesi hiyo amesema kuwa kesi hiyo Kaduna imetuliliwa mbali kutokana na kukiuka mchakato wa kesi nyingine ya shtaka kama hilo inayoshughulikiwa na Mahakama Kuu ya Shirikisho huko Abuja.

Hata hivyo Haruna Magashi, wakili anayemtetea Sheikh Ibrahim Zakzaky amepinga hoja iliyotolewa akisema kuwa kesi hizo mbili kimsingi zinatofautinana na kwamba wanachunguza uamuzi huo wa mahakama ya Kaduna kabla ya kuamua wakate rufaa au la.

Wakilishi wa Sheikh Zakzaky amesisitiza kuwa, kesi ya Abuja inahusu kushikiliwa korokoroni bila ya kufunguliwa mashtaka na kwamba ile ya Kaduna inahusu ukiukwaji wa haki za binadamu ambao hauwezi kushughulikiwa isipokuwa na mahakama ya eneo uhalifu huo ulipotendeka.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 katika kituo cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.

Hivi karibuni Harakati ya Kiislamu Nigeria (INM) ilitahadharisha kuwa kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky huenda akapoteza uwezo wa kuona na kuwa kipofu akiwa kizuizini.

Jeshi hilo lilidai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.

Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ya kiafya si nzuri, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.



3616165

captcha