IQNA

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian

Iran itaendelea kuwaunga mkono Wapalestina kiroho, kisiasa

10:56 - April 24, 2023
Habari ID: 3476906
TEHRAN (IQNA)- Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza azma yake katika kadhia ya Palestina na kusema itaendelea kuwaunga mkono wanamapambano wa Palestina katika kukabiliana na vitendo vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo mapema Jumatatu alipozungumza kwa njia ya simu na Ismail Haniyah, mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, yenye makao yake katika Ukanda wa Gaza.

Akiashiria matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei katika kikao na mabalozi wa nchi za Kiislamu kwa mnasaba wa Idul Fitri siku ya Jumamosi, Amir-Abdollahian amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itaendeleza uungaji mkono wake wa kiroho na kisiasa kwa watu wa Palestina na makundi ya muqawama ambayo yanapigania ukombozi wa Palestina.

Katika kikao cha Jumamosi na wanadiplomasia wa Kiislamu mjini Tehran, Ayatullah Khamenei alisema lengo la ulimwengu wa Kiislamu linapaswa kuwa katika kuwaimarisha wapigania ukombozi wa Palestina katika wakati ambapo Israel inakaribia mwisho wake.

Kiongozi Muadhamu aliashiria kuporomoka hatua kwa hatua kwa utawala haramu wa Israel na kusema: "Uporomokaji huu ambao ulianza miaka kadhaa nyuma umeshika kasi katika wakati huu; na Ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuitumia vizuri fursa hii adhimu".

Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amebainisha, "Kadiri mapambano yanavyoimarika, ndivyo utawala wa Kizayuni unavyozidi kuwa dhaifu, [na] ndivyo ukatili wake unavyozidi kudhihirika. Hali mbaya inayoukabili utawala wa Kizayuni hivi leo ni matokeo ya muqawama wa vijana wa Kipalestina.

Ismail Haniyah, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas kwa upande wake amesisitiza azma kubwa ya wananchi wa Palestina na makundi ya muqawama ya kuendelea na mapambano dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni.

Haniyah pia alipongeza makubaliano ya hivi karibuni kati ya Iran na Saudi Arabia ya kurejesha uhusiano wa kidiplomasia, akisema makubaliano hayo yatazinufaisha nchi zote mbili na eneo zima.

Ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni umekasirishwa mno na makubaliano hayo.

Ikumbukwe kuwa, mnamo Machi 10, baada ya siku kadhaa za mazungumzo mazito yaliyoandaliwa na China, hatimaye Iran na Saudi Arabia zilikubali kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia na kufungua tena balozi zao na ofisi zao za kidiplomasia baada ya miaka saba ya kutokuwa na uhusiano.

4136141

captcha