IQNA

Waislamu Malawi wataka sheria ya kulinda wanawake wanaovaa Hijabu

16:11 - October 01, 2015
Habari ID: 3377130
Waislamu nchini Malawi wanataka kuwepo sheria za kuwalinda wanawake Waislamu wanaovaa vazi la stara la Hijabu ili wasibaguliwe wala kubughudhiwa katika maeneo ya umma na kazini.

"Kumekuwepo na kesi za kudhulumiwa na kubaguliwa vibaya wanawake Waislamu katika maeneo yao umma na kazini; hili linafanyika kwa sababu hakuna sheria za kutulinda huku wanaotekeleza vitendo hivyo wakiachwa kutembea huru na waathirika wakiumia pasina kuwa na uwezo wa kufanya lolote," amesema Fatima Ndaila, Mwenyekiti Taifa wa Jumuiya ya Wanawake Waislamu (MWO).
Katika mahojiano na tovuti ya OnIslam.net ameongeza kuwa: "Ni kwa sababu hii ndio tunataka sheria za kutulinda.  Kwa nini iwe rahisi kuwasumbua wanawake wenye hijabu?
"Wanawake wenye hijabu wanakabiliana na ubaguzi mkubwa. Tunatizamwa kwama watu waliobaki nyuma kimaendeleo. Wakati wa mahojiano ya kutafuta ajira, tunalazimishwa kuvua hijabu. Hii ni kejeli kwa dini yetu," aliongeza Ndaila.
Mbunge pekee mwanamke Mwislamu Malawi, Aisha Mambo anaafikiana na Ndala na kusema wanawake Waislamu wanaovaa hijabu wanabaguliwa. Hatahivyo ana wasi wasi mkubwa kuhusu kutofanikiwa pendekezo la kuptisha sheria ya kuwalinda wanawake Waislamu wanaovaa hijabu kutokana na idadi ndogo ya wabunge Waislamu.
Tokea mwaka 1993 wakati Bakili Muluzi alipochaguliwa kuwa rais wa kwanza Mwislamu Malawi, kulishuhudiwa ongezeko la wanawake wanaovaa hijabu katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika. Waislamu ni takribani asilimia 36 ya watu wote milioni 15 nchini Malawi..../mh

3375712

captcha