IQNA

Gingrich, Spika wa Zamani wa Bunge la Marekani

Waislamu wenye Imani Thabiti ya Kiislamu Wafukuzwe Marekani

11:59 - July 16, 2016
Habari ID: 3470456
Spika wa zamani wa Kongresi ya Marekani amesema kuwa Waislamu wanaoshikamana na sheria za Kiislamu wanapaswa kufukuzwa nchini Marekani.

 Katika mahojiano n kanali ya televisheni ya Fox News yenye misimamo mikali, Newt Gingrich amesema kunapaswa kufanyike upelelezi kuhusu historia ya Waislamu wanaoishi Marekani na Waislamu wote wanaoshikamana na sheria za dini hiyo wafukuzwe nchini Marekani.

Mwanasiasa huyo mwenye misimamo ya kufurutu ada amesema, ustaarabu wa Magharibi umo katika vita, hivyo kuna udharura wa kufanyika uchunguzi kuhusu historia ya kila Mwislamu anayetekeleza vyema mafundisho yake na iwapo hilo litathibitika afukuzwe Marekani. Spika wa zamani wa Bunge la Marekani amedai kuwa sheria za Kiislamu hazioani na ustaarabu wa Magharibi.

Newt Gingrich amesema, kwanza Waislamu wanapaswa kusailiwa, kisha kufanyike uchunguzi kuhusu wanayoyafanya katika mtandao wa intaneti na baadaye misikiti yao idhibitiwe.

Gingrich amesema hayo wakati wa kuzindua kampeni za mgombea mtarajiwa wa kiti cha rais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican Donald Trump.

Mwaka uliopita Donald Trump mwenyewe alitoa wito wa kuzuiliwa Waislamu kuingia Marekani na kutoa pendekezo la kutumiwa mbinu za manazi wa Ujerumani dhidi ya wafuasi wa dini hiyo.

3515150

captcha