IQNA

Viongozi wa Waislamu Marekani wajibu matamshi ya chuki ya Trump

23:26 - December 06, 2016
Habari ID: 3470721
IQNA-Viongozi wapatao 300 wa jamii ya Waislamu nchini Marekani wamemwandikia barua ya wazi Rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump likiwa ni jibu kwa matamshi ya chuki aliyotoa dhidi ya Uislamu.
Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, viongozi 291 wakiwemo wajumbe wakuu wa Baraza la Mahusiano ya Marekani na Uislamu (CAIR), maimamu wa misikiti, wahadhiri wa vyuo vikuu, wanaharakati pamoja na wakuu wa jumuiya za Kiislamu wamemwandikia barua ya wazi rais mteule wa nchi hiyo Donald Trump na mawaziri wote wa serikali yake kuwataka waheshimu sheria za nchi.

Barua hiyo ya Waislamu wa Marekani kwa rais mteule wa nchi hiyo imeandikwa kufuatia ripoti kwamba Trump amepanga kuanzisha mfumo wa uchunguzi, udhibiti na usajili wa taarifa za Waislamu. 

Vitendo vya utumiaji nguvu dhidi ya Waislamu vimeshtadi nchini Marekani baada ya Donald Trump kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo. Viongozi wa Waislamu nchini humo wanaitakidi kuwa kauli zilizokuwa zikitolewa na Trump katika kipindi cha kampeni za uchaguzi ndizo zilizosababisha kuongezeka hisia za chuki dhidi ya Uislamu.

Itakumbukwa kuwa miongoni mwa ahadi ambazo Donald Trump aliahidi kuzitekeleza baada ya kushinda uchaguzi wa rais ni kuzuia wahajiri Waislamu kuingia nchini Marekani.

Halikadhalika kumeshuhudiwa wimbi la hujuma dhidi ya Waislamu kote Marekani baada ya Donald Trump kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais  uliofanyika Novemba 8.

Kwa mujibu Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR), ambalo hutetea haki za Waislamu, mbali na wanawake Waislamu kushambuliwa pia kumeshuhudiwa hujuma dhidi ya watoto Waislamu.

"Hii ni natija ya chuki dhidi ya Uislamu kuwa sera rasmi kama ambavyo tumeshuhudia miezi ya hivi karibuni katika kampeni za uchaguzi wa rais,” amesema msemaji wa CAIR Ibrahim Hooper. Aidha amesema ni jukumu la Trump kulaani ubaguzi na chuki dhidi ya Uislamu. Hadi sasa Trump au wapambe wake hawajatoa taarifa yoyote kuhusu kuongezeka hujuma dhidi ya Waislamu Marekani.

3551444


captcha