IQNA

Jitihada za Waislamu Marekani kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

1:25 - June 07, 2016
Habari ID: 3470364
Waislamu nchini Marekani katika jimbo la New Mexico wametangaza kuimarisha harakati za kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia).
Taasisi ya Kiislamu ya 'Rain Drop' imekuwa ikiendesha harakati pana kwa ajili ya kuwafahamisha wakazi wa mji huo kuhusu dini ya Kiislamu na kukabiliana na propaganda na vitendo vya chuki dhidi ya wafuasi wa dini hiyo. Kwa mujibu wa habari hiyo, katika harakati hizo Waislamu wa mji huo wamekuwa wakifanya vikao na mikutano ya hadhara katika vyuo vikuu, makanisa na katika maktaba za mji huo. Nasib Orhan, mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo ya Rain Drop ambayo ilifunguliwa miaka sita iliyopita mjini New Mexico amenukuliwa akisema kuwa, hivi sasa wanajitahidi kufikisha mjini hapo ujumbe wa amani, majadiliano, kuheshimu itikadi za wengine, kuishi pamoja kwa amani na kuheshimiana. Akiashiria matamshi ya chuki ya baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini Marekani, hususan matamshi ya ubaguzi ya Donald Trump, mgombea wa kiti cha urais kwa chama cha Republican kwenye uchaguzi mkuu ujao, amesema kuwa matamshi hayo ni ya kusikitisha sana na kusisitiza kuwa, licha ya mwanasiasa huyo kutafuta uungaji mkono kupitia nara za chuki, lakini wakazi wa mji wa Albuquerque hawajamkubali. Orhan amesema kuwa, ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana taasisi hiyo ya Kiislamu ikaongeza jitihada zake katika kukabiliana na mienendo kama hiyo dhidi ya Uislamu. Kwa mujibu wa takwimu karibu Waislamu 4.000 wanaishi katika jimbo la New Mexico nchini Marekani.
captcha