IQNA

Hofu baada ya Trump kuwateua maafisa wenye chuki dhidi ya Uislamu

16:42 - November 19, 2016
Habari ID: 3470684
IQNA-Rais-mteule wa Marekani Donald Trump amewateua watu wenye chuki dhidi ya Uislamu kuhudumu katika Ikulu ya White House jambo linanloashiria muendelezo wa sera zake za chuki ambazo zimewatia hofu Waislamu nchini humo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Siku ya Ijumaa mashirika ya kijamii na viongozi wa Waislamu Marekani walitangaza bayana wasiwasi wao kuhusu hatua ya Trump kuwateua watu wenye chuki dhidi ya Uislamu katika nyadhifa muhimu za usalama wa taifa.

Hata baadhi ya maafisa wa serikali ya sasa na zilizopita Markenai wamebainisha wasi wasi wao kuwa watu walioteuliwa na Trump wataupa nguvu mtazamo wa Waislamu kuwa Marekani inaendesha vita dhidi ya dini ya Uislamu. Tokea Trump atangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais wa Mareknai, kumeshuhudiwa wimbi la hujuma dhidi ya Waislamu na watu wa jamii za wachace nchini humo.

Ijumaa, afisa mstaafu katika Jeshi la Mareknai Luteni Jenenrali Michale Flynn alikubali uteuzi wa Trump wa kuhudumu kama mshauri wa usalama wa taifa. Flynn ana historia ya kutoa matamshi makali dhidi ya Uislamu. Naye Seneta Jeff Session amekubali uteuzi wa Trump wa kuwa mwanasheria mkuu Marekani. Seneta huyo anaunga mkono kauli ya Trump ya kutaka kuzuiwa Waislamu kuingia Marekani. Aidha Trump amemteua mjumbe wa Congress, Mike Pompeo kuwa mkuu wa Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani, CIA. Pompeo amekuwa akitoa madai kuwa viongozi wa Waislamu Marekani hawachukui misimami imara dhidi ya ugaidi. Halikadhalika anapinga vikali mapatano ya nyuklia baina ya Iran na madola sita makubwa duniani. Ibrahim Hooper Msemaji wa Baraza la Mahusiano ya Uislamu na Marekani CAIR amesema ni jambo la kushangaza kuona watu wenye chuki dhidi ya Uislamu wakipewa nafasi muhimu katika serikali ya Trump.

Naye Talib M. Shareef, ambaye ni Imamu na mwenyekiti wa Masjid Muhammad mjini Washington, msikiti mkongwe zaidi Marekani, amesema Wamarekani wote wanapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu watu walioteuliwa na Trump. Shareef ambaye amewahi kuhudumu katika Jeshi la Marekani amesema uteuzi wa Flynn, Sessions na Pompeo ni jambo ambalo litapelekea Marekani kutengwa na waitifaki wake na pia kuwatia wasiwasi Waislamu hasa wanaohudumu jeshini na katika serikali.

Trump hadi sasa anawateua watu wenye misimamo yake ya kibaguzi na chuki dhidi ya wahajiri wa kigeni hasa watu wenye asili ya Afrika na Waislamu.

Tayari mkurugenzi mtendaji wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch Kenneth Roth amemuonya Trump, kuhusu utendaji kazi wake baada ya kuingia madarakani.

3547146

captcha