IQNA

Migongano baada ya ISIS kutangaza kinara mpya wa Boko Haram

6:55 - August 05, 2016
Habari ID: 3470495
Baada ya kundi la kigaidi la ISIS kutangaza kuteua kinara mpya wa kundi la kigaidi la Boko Haram, kumeibuka hitilafu huku kinara wa muda mrefu wa Boko Haram akipinga uteuzi huo.

Abubakar Shekau, kinara wa kundi la kitakfiri la Boko Haram Alhamisi alituma uumbe wa sauti kupinga hatua ya juzi ya ISIS au Daesh kumtangaza Abu Mus'ab al Barnawi kuwa kinara wa kundi hilo la kitakfiri magharibi mwa Afrika. Shekau ambebaini kuwa, wanachama wa Boko Haram hawamkubali mtu yoyote kuwa kiongozi wao mpya.

Shekau ambaye amekuwa kinara wa Boko Haram tangu mwaka 2009 ametangaza kuwa watu wanapaswa kuelewa kuwa kundi la Boko Haram bado lipo na kwamba limepinga uamuzi huo wa ISIS wa kumuuzulu. Itakumbukwa kuwa mwezi Machi mwaka jana kundi la Boko Haram lilitangaza utiifu kwa kundi la kigaidi la ISIS. Aidha hivi karibuni kuliibuka tetesi kuwa Abubakar Shekau ameuawa huku jeshi la Nigeria likitangaza mara kadhaa kumuua kinara huyo wa Boko Haram. Abu Mus'ab al Barnawi alikuwamsemaji wa kundi la Boko Haram.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa inayotumiwa na Waislamu wengi Nigeria lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo na pia katika nchi jirani. Tokea kundi hilo lianzisha uasi mwaka 2009 hadi sasa, takribani watu 20,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili kukimbia makazi yao.

3520075

captcha