IQNA

Magaidi wa Boko Haram waua Waislamu 22 msikitini Nigeria

18:24 - March 16, 2016
Habari ID: 3470201
Magaidi wakufurishaji wa kundi la Boko Haram nchini Nigeria wamewaua watu 22 waliokuwa wakisali katika msikiti mmoja jimboni la Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Afisa mmoja wa usalama katika jimbo hilo na ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema kuwa, watu hao wameuawa katika shambulizi la kujiripua lililofanywa na gaidi mwanamke wa genge hilo lenye kufuata itikadi potovu za Kiwahabi katikati ya watu waliokuwa wakisali msikitini. Baada ya shambulio hilo, gaidi mwingine wa kike aliyekuwa amevalia mada za miripuko alijiripua nje ya msikiti wakati watu walipokuwa wakikimbia kutoka msikitini kuokoa maisha yao. Watu wasiopungua 22 wamepoteza maisha eneo la tukio huku wengine 17 wakijeruhiwa na wengine hali zao ni mahututi. Siku chache zilizopita wanachama wa genge hilo lililotangaza kiapo chake kwa kundi la kitakfiri la ISIS au Daesh, lilifanya shambulizi lingine katika jimbo la Kano kaskazini mwa nchi hiyo na kuua watu watatu na kujeruhi wengine wapatao saba.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa inayotumiwa na Waislamu wengi Nigeria lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo. Tokea kundi hilo lianzisha uasi mwaka 2009 hadi sasa, takribani watu 20,000 wameuawa na wengine takribani milioni mbili kukimbia makazi yao.

3483906

captcha