IQNA

Waislamu Marekani walaani shambulizi la kisu Chuo Kikuu Ohio

17:58 - November 29, 2016
Habari ID: 3470704
IQNA-Viongozi wa jamii ya Waislamu Marekani wamelaani vikali hujuma ya kigaidi katika jimbo la Ohio, ambapo mwanafunzi mmoja wa Marekani mwenye asili ya Somalia aliwashambulia kwa kisu wanachuo wenzake.

Taarifa ya Baraza la Mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani CAIR imelitaja tukio hilo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Ohio kama la kuhuzunisha na la kuvunja moyo.

Jana Jumatatu, kijana Mmarekani mwenye asili ya Kisomali kwa jinaAbdul Razak Ali Artan mwenye umri wa miaka 18, aliwakanyaga kwa makusudi wapita njia kwa gari lake katika jimbo la Ohio, kabla ya kuingia katika chuo kikuu cha jimbo hilona kujeruhi watu 11 kwa kuwadunga kisu.

Hata hivyo mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Ohio ambaye alikuwa mkimbizi kutoka Somalia, aliuawa na maafisa wa polisi kwa kufyatuliwa risasi baada ya kufanya hujuma hiyo.

Roula Allouch, Mwenyekiti wa bodi ya taifa ya baraza hilo amesema watu wanaotekeleza hujuma za aina hiyo hawatumi ujumbe dunianikwa niaba ya Waislamu na kwamba mamilioni ya Waislamu nchini Marekani na mabilioni yao kote duniani wanalaani ukatili wa namna hii.

Naye Jennifer Nimer, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria wa baraza hilo katika jimbo la Ohio amesema, na hapa tunamnukuu: "Tunalaani vikali kitendo hicho kisicho cha utu".

Kumeshuhudiwa wimbi la hujuma dhidi ya Waislamu kote Marekani baada ya Donald Trump kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi wa rais mapema mwezi huu.

3549900

captcha