IQNA

Walowezi wa Kizayuni wauvamia na kuuvunjia heshima tena Msikiti wa Al Aqsa

23:16 - April 14, 2017
Habari ID: 3470934
TEHRAN (IQNA)-Walowezi wa Kizayuni wakisaidiwa na kupewa ulinzi na askari polisi wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel wamevamia tena na kuuvunjia heshima msikiti wa Al-Aqsa na wa Haram ya Nabii Ibrahim AS.
Alkhamisi alfajiri, mamia ya wazayuni, wakisindikizwa na vikosi vya polisi ya Israel waliuvamia msikiti wa Al–Aqsa kupitia mlango wa Babul-Maghaaribah katika mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na vilevile wakavamia msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim (as) katika mji wa Al-Khalil kusini mwa Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.

Maeneo hayo matakatifu yamegeuzwa uwanja wa kujifaragua askari na walowezi wa Kizayuni na kutekeleza njama yao ya kufuta utambulisho wa Kiislamu wa maeneo ya Palestina na kuweka badala yake nembo za Kizayuni. Kushtadi vitendo vya hujuma na uvunjiaji heshima vya Wazayuni dhidi ya msikiti mtukufu wa Al-Aqsa na wa Haram ya Nabii Ibrahim kunajiri katika hali ambayo maeneo matakatifu katika ardhi za Palestina inayokaliwa kwa mabavu yamekuwa kila mara yakiandamwa na hujuma na mashambulio ya utawala haramu wa Israel.

Njama za kuyahudisha maeneo ya Waislamu

Kwa kuzingatia kwamba utawala wa Kizayuni unafanya kila hila ili kubadilisha utambulisho wa kidini wa ardhi unazozikalia kwa mabavu na kuziyahudisha kikamilifu ardhi hizo, maeneo ya kidini ambayo ni sehemu ya utambulisho wa kidini wa Wapalestina ndiyo yanayopewa kipaumbele cha kwanza katika kampeni hiyo ya Uyahudishaji.

Walimwengu wangali wanakumbuka tukio la tarehe 21 Agosti mwaka 1969 la kuchomwa moto msikiti wa Al-Aqsa. Kibla hicho kwa kwanza cha Waislamu na moja ya maeneo matakatifu yanayoheshimiwa na dini za mbinguni kilihujumiwa na mzayuni mmoja mwenye misimamo ya kufurutu mpaka aitwaye Denis Michael Rohan. Hujuma hiyo ya uchomaji moto ilisababisha hasara kubwa kwa sehemu kadhaa za msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Katika tukio jengine la tarehe 25 Februari mwaka 1994, mzayuni mwengine aitwaye Baruch Goldstein alivamia msikiti wa Haram ya Nabii Ibrahim (as) na kuwafyatulia risasi waumini waliokuwa wakisali ndani yake, akawaua shahidi Wapalestina 29 na kuwajeruhi wengine 150. Na baada ya shambulio hilo la umwagaji damu utawala wa Kizayuni ukashadidisha zaidi sera za kulidhibiti eneo hilo takatifu kama ulivyofanya kuhusiana na msikiti wa Al-Aqsa.

Masinagogi 100 kando ya Msikiti wa Al Aqsa

Baada ya shambulio la Wazayuni katika haram ya Nabii Ibrahim AS, eneo hilo liligawanywa sehemu mbili, lengo likiwa ni kuufanya utawala ghasibu uidhibiti sehemu kubwa ya haram hiyo kwa kuendeleza ukaliaji wake wa mabavu, kusababisha hali ngumu ya maisha kwa wananchi wa Palestina na kuweka kambi za Kizayuni kwa madhumuni ya kuidhibiti kikamilifu haram hiyo.

Aidha tangu msikiti mtukufu wa Al-Aqsa ulipochomwa moto hadi sasa, utawala haramu wa Israel umekuwa ukifanya kila njama ili kufanikisha ndoto yake ya kuubomoa kikamilifu msikiti huo mtukufu, ambapo hatua kwa hatua umekuwa ukitekeleza mipango ya kukiyahudisha kikamilifu kibla hicho cha kwanza cha Waislamu na kubadilisha muundo wake wa Kiislamu na Kiarabu. Uchimbaji mkubwa wa mashimo ya chini ya ardhi chini ya msikiti wa Al-Aqsa unaoendelea hadi sasa ni hatari kubwa inayotishia uwepo wa mahala hapo patakatifu. Wazayuni aidha wameuzingira msikiti huo kwa kujenga masinagogi yapatayo 100 pamoja na vituo vingine vya kiyahudi.

Kitendo cha Israel cha kufuta athari yoyote ile ya Kiislamu na kihistoria ya taifa la Palestina na kubadilisha muundo wa kijiografia na wa idadi ya watu kandokando ya maeneo hayo inalenga kupachika badala yake alama na nembo bandia katika ardhi ya Wapalestina. Utawala wa Kizayuni umekuwa ukitekeleza kila mara sera ya kuyapa sura ya Kizayuni maeneo ya ardhi za Palestina kwa kupotosha ukweli wa mambo kwa njia ya kubomoa turathi za Kiislamu, nyumba na majengo ya kihistoria ya Wapalestina na kujenga badala yake mahekalu ya kiyahudi.

UN yauonya utawala wa Israel

Hii ni katika hali ambayo, maazimio nambari 242 na 338 ya Umoja wa Mataifa pamoja na mkataba wa nne wa Geneva yameuonya utawala wa Kizayuni kwa kuutaka ujiepushe na kuyatwaa na kuyatumia kwa namna yoyote ile maeneo ya ardhi za Palestina unayoyakalia kwa mabavu. Jinai za utawala habithi wa Israel za kubomoa na kuyavunjia heshima maeneo na majengo ya Kiislamu na kuyadhibiti maeneo hayo kwa lengo la kuwafukuza Wapalestina wote katika mji mtakatifu wa Baitul Muqaddas na maeneo mengine ya Palestina vinadhihirisha sera za kibaguzi za utawala huo ghasibu za kukabili na uhuru wa kuabudu wa wafuasi wa dini hizo za mbinguni, na na dini za Mwenyezi Mungu.

3462572



captcha