IQNA

Msikiti wa Jamia Paris

Ushindi wa Macron waibua matumaini miongoni mwa Waislamu Ufaransa

13:59 - May 08, 2017
Habari ID: 3470972
TEHRAN (IQNA)-Msikiti wa Jamia wa mjini Paris umekaribisha ushindi wa Emmanuel Macron kama rais wa Ufaransa.

Katika taarifa siku ya Jumapili, wakuu wa msikiti huo wamesema ushindi wa Macron, mwenye misimamo ya wastani, dhidi ya kiongozi wa mrengo wa kulia mwenye misimamo mikali Bi. Marine Le Pen ni ishara ya maelewano miongoni mwa wafuasi wa dini mbali mbali Ufaransa.

"Msikiti wa Jamia wa Paris unautazama ushindi huu kama ishara ya maelewano baina ya wafuasi wa dini mbali mbali ili kukabiliana na vitisho vinavyoukabili umoja wa taifa," taarifa hiyo imesema.

Msikiti huo ambao Kifaransa unajulikana kama La Grande Mosquée de Paris umesema: "Ni ishara ya matumaini kwa Wafaransa kuwa wanaweza kuishi kwa maelewano na kuheshimu thamani za Kifaransa."

Katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliofanyika Jumapili, Macron alimuacha mbali mpinzani wake Le Pen kwa kujinyakulia asilimia 66 ya kura. Le Pen amepata asilimia 34.9 ya kura. Maelfu ya wanaomuunga mkono Macron walijitokeza katika mitaa na barabara katikati mwa Paris wakipeperusha bendera. Akiwa na miaka 39, Macron anakuwa raia mwenye umri wa chini zaidi kuwahi kuchaguliwa nchini Ufaransa na wa kwanza kuchaguliwa kutoka nje ya vyama viwili vikubwa nchini humo.

Le Pen amekuwa na misimamo mikali sana dhidi ya Waislamu na amewashi kusema Waislamu wanaoswali barabarani wakati misikiti imejaa ni sawa na wanazi walioikalia Ufaransa kwa mabavu. Akihutubia mkutano wa kampeni hivi karibuni, Macron alisema chama cha Le Pen ni cha chuki na kuongeza kuwa: "Sitaruhusu watu watusiwe tu kwa ajili wanaamini Uislamu." Aidha Macron ameripotiwa kupinga marufuku ya Hijabu katika vyo vikuu vya Ufaransa.

3462769
captcha