IQNA

Maelfu waandamana Ujerumani kupinga ugaidi

12:57 - June 18, 2017
Habari ID: 3471023
TEHRAN (IQNA)-Maelfu ya watu, wengi wao wakiwa Waislamu, wameandamana katika mji wa Cologne magharibi mwa Ujerumani kupinga ugaidi unaotendwa kwa jina la Uislamu.

Waandamanaji walimiminika katika mitaa ya Cologne Jumamosi katika sehemu ya 'Matembezi ya Amani' kwa lengo la kutoa wito kwa watu kote duniani waungane kupambana na ugaidi.

Maandamano hayo yamewaleta pamoja washiriki zaidi ya 3,500 pamoja na kuwa kulikuwa na joto kali huku wengi wakiwa katika saumu ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Washiriki walikuwa wamebeba mabango yaliyoandikwa, "Pamoja Dhidi ya Ugaidi", na "Ugaidi Hauna Dini."

Walioandaa maandamano hayo wanasema lengo lao lilikuwa ni kufikisha ujumbe huu kuwa, Waislamu hawaungi mkono misimamo mikali na ugaidi hasa baada ya nchi kadhaa za Ulaya, zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Ubelgiji kulengwa na magaidi wanaofungamana na kundi la ISIS. Aidha washiriki wamebainisha masikitiko yao kuwa hujuma hizo za kigaidi zinatekelezwa na watu ambao wanatetea vitendo vyao kwa kutumia jina la Uislamu katika hali ambayo dini hii tukufu inapinga vitendo kama hivyo.

Maandamano hayo yalileta pamoja mashirika kadhaa ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na Baraza Kuu la Waslamu Ujerumani. Kuna takribani Waislamu milioni nne Ujerumani ambao ni asilimia tano ya watu wote wa nchi hiyo ya Ulaya magharib.

Ujerumani imekuwa katka hali ya tahadhari tokea Julai mwaka 2016 baada ya hujuma za kigaidi kupelekea watu 15 kupoteza maisha wakiwemo washambuliaji.

captcha