IQNA

Ujerumani yaruhusu adhana kupitia vipaza sauti mjini Cologne

16:39 - October 11, 2021
Habari ID: 3474410
TEHRAN (IQNA)- Wakuu wa Ujerumani wameruhusu adhana kupitia vipaza sauti wakati wa Sala ya Ijumaa katika mji wa Cologne wenye Waislamu wengi.

Kwa mujibu wa taarifa idhini hiyo imetolewa kwa majaribio kwa muda wa miaka miwili.

Meya wa Mji wa Cologne Henriette Reeker amesema wametoa idhini hiyo kufuatia maombi ya Waislamu mjini humo na kwamba adhana itaruhusiwa kupitia vipaza sauti kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa.

"Raia wetu Waislamu ni sehemu ya wakazi wa mji huu. Kusikia sauti ya adhana sambamba na kengele za makanisa katika mji wetu ni dhihirisho kuwa uwepo wa watu wa jamii mbali mbali uko nasi na ni jambo la kujivunia," amesema Henriette.

Kwa mujibu wa idhini iliyotolewa, adhana haipaswi kuwa zaidi ya dakika 10 na pia sauti ya vipaza sauti iwe ya wastani.

Aidha wakati wa Adhana lazima kuwepo na mtu ambaye atawajibika msikitini iwapo kutakuwa na malalmiko.

Mwaka 2018, mahakama moja ya Ujerumani ilipiga marufuku  Adhana wakati wa sala ya Ijumaa baada ya malalamikio ya familia moja ya Wakristo waliokuwa wakiishi karibu kilomita moja kutoka msikiti walioulalamikia.

Ingawa mwaka jana wasimamizi wa mji mkuu Berlin waliruhusu adhana wakati wa kilele cha janga la COVID-19 ili kuinua motisha miongoni mwa wakazi lakini baada walipiga marufuku tena kwa kisingizo kuwa misikiti ilikuwa imefungwa kutokana na janga hilo.

3475987

captcha