IQNA

Mufti Mkuu wa Misri

Daesh ni magaidi wanaovunja thamani za Kiislamu

18:55 - August 14, 2014
Habari ID: 1439297
Mufti Mkuu wa Misri amesema kuwa vitendo vinavyofanywa na kundi la Daesh vinapingana na thamani za kibinadamu na Kiislamu na kwamba kundi hilo ni genge la kigaidi ambalo haliwezi kutambuliwa kuwa ni dola la Kiislamu.

Mufti Mkuu wa Misri Shauqi Allam ametoa wito wa kuwepo ushirikiano wa kikanda na kimataifa kwa shabaha ya kukabiliana na vitendo vya kundi la Daesh na makundi mengine ya kigaidi. Amesema kuwa kundi la kigaidi la Daesh mbali na kukanyaga thamani za Kiislamu na malengo aali ya sheria yaliyowekwa na dini ya Uislamu, limekiuka pia thamani za kibinadamu zinazowakutanisha pamoja wanadamu wote.

Mufti Mkuu wa Misri amesema Daesh na makundi mengine ya kigaidi ni hatari kubwa kwa Uislamu na Waislamu na kuongeza kuwa, makundi hayo yanachafua sura ya Uislamu kama ambavyo yanamwaga damu za watu wasio na hatia na kueneza ufuska na ufisadi. Ameongeza kuwa vitendo vya kundi hilo vinadhoofisha mataifa na nchi za Kiislamu na kutayarisha uwanja mzuri wa maadui kuingilia mambo ya ndani ya Waislamu kwa kisingizio cha vita dhidi ya ugaidi.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Idara ya Fatuwa ya Misri (Darul Iftaa) imezitaja jinai zinazofanywa na kundi la Daesh huko Iraq kuwa ni jinai dhidi ya binadamu na kwamba hatua za kundi hilo zinapingana na mafundisho ya Uislamu. Kituo hicho cha juu cha kidini nchini Misri pia kimekuwa kikisisitiza juu ya udharura wa kupambana na kundi hilo la kigaidi la Daesh na makundi mengine yenye misimamo ya kufurutu mipaka.

1438878

Kishikizo: daesh kiislamu mufti misri
captcha