IQNA

EU kuuongezea vikwazo utawala haramu wa Israel

23:03 - November 19, 2014
Habari ID: 1475311
Kamati ya Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya imetangaza vikwazo vipya dhidi ya utawala wa Israel kutokana na hatua za utawala huo za kuvuruga usalama wa Baitul Maqdis na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Tokea Januari mwaka huu wa 2014 Umoja wa Ulaya ulianza kutekeleza vikwazo dhidi ya utawala wa Kizayuni. Gazeti la Kizayuni la Haaretz limewanukulu wanadiplomasia wa Ulaya na maafisa wa ngazi za juu wakisema kuwa, wiki tatu zilizopita  Kamati ya Sera za Kigeni katika Umoja wa Ulaya  iliwasilisha waraka wa siri mbele ya wawakilishi 28 wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambao ulitathminiwa kuwa ni rasimu ya mpango mpya wa umoja huo wa kuuwekea vikwazo utawala wa Israel.

Vikwazo hivyo vipya vya Umoja wa Ulaya ni jibu kwa hatua ya Baraza la Mawaziri la Israel ya kupuuza na kutotilia maanani onyo lililotolewa na jamii ya kimataifa. Adhabu na vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Israel ni pamoja na kususia bidhaa zilizozaliswa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kupunguza ushirikiano na utawala wa Kizayuni katika nyuga za uchumi na kubatilisha mapatano ya ushirikiano wa biashara huru na utawala huo.

Umoja wa Ulaya umeweka sharti la kuboresha uhusiano wake na utawala wa Kizayuni kuwa ni utawala huo kuchukua hatua za kusogeza mbele mazungumzo na Wapalestina kwa  lengo la kupatikana suluhisho litakalopelekea kuundwa nchi huru ya Palestina. Kwa mujibu wa waraka huo wa siri Umoja wa Ulaya aidha unataka kupunguza kiwango cha uhusiano wake na utawala wa Israel. Imedokezwa kuwa waraka huo umetayarishwa na Christian Berger mkuu wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Kamati ya Sera za Kigeni ya Umoja wa Ulaya. Mwaka uliopita Berger pia aliwasilisha pendekezo la kuwekewa vikwazo bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Katika siku za hivi karibuni miji mbali mbali kote Ulaya imeshuhudia maandamno makubwa ya watu kwa ajili ya kutetea Masjidul Aqsa na mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds Tukufu. Waandamanaji sambamba na kupinga hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa na mji wa Quds, pia wametaka jamii ya kimataifa ingilie kati na kuzuia hujuma  hizo hasa ujenzi wa vitongoji vya  walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Wananchi wa ulaya katika miji ya London, Paris, Stockholm, Roma, Vienna na miji mingine mikubwa ya Ulaya wameandamana kwa mnasaba wa  'Wiki ya Kuunga Mkongo Al Aqsa Ulaya". Katika maandamano yao watu wa Ulaya wametangaza himaya yao kwa Msikiti wa Al Aqsa  huku wakilaani vikali hujuma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya eneo hilo tukufu. Katika miezi ya hivi karibuni mji wa Baitul Maqdis umeshuhudia makabiliano makali baina ya Wapalestina na askari wa utawala wa Kizayuni. Wapalestina wamekuwa wakilalamikia hujuma za mara kwa mara za Wazayuni dhidi ya Msikiti wa Al Aqsa na kuwekwa vizingti dhidi ya Waislamu wanaotaka kuswali katika msikiti huo. Aidha Wapalestina wanalalamikia hatua ya utawala wa Israel ya kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya Wazayuni katika Quds Tukufu na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Hivi sasa kumeibuka wimbi kubwa la malalamikio dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kote duniani kutokana na suala hilo. Walimwengu wameandamana kwa lengo la kulaani maovu ya Israel katika mji wa Quds na Msikiti wa Al Aqsa. Aidha waliowengi duniani wametangaza kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa. Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni huko Ulaya unaonyesha kuwa hisia dhidi ya Utawala wa Kizayuni wa Israel zimengoezeka barani humo hasa baada ya jinai za utawala huo katika vita vyake vya hivi karibuni dhidi ya Ghaza. Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa maazimio 143 dhidi ya Israel katika nchi 10 za Ulaya.

Utawala wa Kizayuni wa Israel umekalia kwa mabavu ardhi za Palestina kwa miaka 66 sasa na hivi sasa unakabiliwa na hasira za watu wa mataifa mengi duniani ambao wanataka serikali zao ziuwekee vikwazo na kuuadhibu utawala huo bandia kutokana na jinai zake dhidi ya Wapalestina.../mh

1474822

captcha