Akizungumza na gazeti la al Ahram linalochapishwa nchini Misri, Mufti Mkuu wa nchi hiyo amesisitiza kwamba dini ya Kiislamu imeweka misingi na sheria za kuhifadhiwa haki za mateka na kwamba Mtume Mtukufu (saw) daima alikuwa akiwausia Masahaba zake kuamiliana vyema na mateka. Mufti Mkuu wa Misri ameongeza kuwa wanamgambo wa kitakfiri na kigaidi wa Daesh wamekuwa wakiwauwa Waislamu kwa kuwakata vichwa na kuwachoma moto mateka wanaowashikilia, jambo ambalo ni kinyume na mafundisho ya Kiislamu. Sheikh Shawki Ibrahim Allam ameongeza kuwa, Mtume Mtukufu (saw) amesema kuwa, Mwenyezi Mungu ameharamisha kumwagwa damu ya mtu aliyetoa shahada ya kumuamini Mwenyezi Mungu mmoja na Muhammad (saw) ni Mtume wake, lakini magaidi wa Daesh wamekuwa wakiendeleza vitendo vya kikatili vya kuuawa, kubaka na kunajisi Waislamu na wasio Waislamu katika nchi za Syria na Iraq..../MH