IQNA

Washiriki kutoka nchi 70 katika kikao Umoja wa Kiislamu Tehran

7:28 - December 23, 2015
Habari ID: 3468455
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema mkutano wa kimataifa wa Umoja wa Kiislamu utafanyika mjini Tehran kuanzia tarehe 27-29 mwezi Desemba.

Ayatullah Muhsin Araki ameyasema hayo alipohutubia mkutano na waandishi habari mjini Tehran Jumanne hii na kuongeza kuwa mkutano wa mwaka huu utakuwa na washiri wa kigeni zaidi ya 300 wakiwemo wasomi na wanazuoni wa Kiislamu kutoka nchi 70 za mabara ya Amerika,  Asia, Afrika na Ulaya. Mbali na wanazuoni wa Kiislamu pia mkutano huo utahudhuriwa na mawaziri, maspika wa mabunga, wakuu wa vyuo vikuu na mamufti wa nchi kadhaa za Kiislamu.
Ayatullah Araki ameongeza kuwa mkutano wa mwaka huu utajadili mada kuu ya "Migogoro ya Sasa Katika Ulimwengu wa Kiislamu" na kwamba kongamano hilo linafanyika katika wakati wa Maulidi ya Mtume Muhammad SAW na Wiki ya Umoja wa Waislamu.
Ayatullah Araki amesema mkutano wa mwaka huu utakuwa na kamati 12 ambazo zitajadili masuala kama vile sayansi na teknolojia, vyuo vikuu, utatuzi wa migogoro, tathmini ya migogoro katika ulimwengu wa Kiislamu na njia za kujikwamua, muqawama, fmailia, wanawake, biashara na vijana.
Aidha amesema kikao cha mwaka huu kitaangazia pia suala la vijana duniani ambapo kuna mkakati maalumu wa kueneza barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa vijana wa nchi za Magharibi.
Waislamu duniani wako katika mwezi mtukufu wa kuadhimisha Maulid ya Mtume Mtukufu wa Uislamu Mohammad al Mustafa SAW. Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaadhimisha siku hiyo tarehe 12 Rabiul Awwal na Waislamu wa Madhehebu ya Shia wanamini siku hiyo ni tarehe 17 Rabiul Awwal.
Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu.

3468244

captcha