IQNA

Mjukuu wa Mandela asilimu na kufunga ndoa na binti Mwislamu

21:38 - February 10, 2016
Habari ID: 3470128
Mandla Mandela, mjukuu wa kiongozi wa zamani wa Afrika Kusini hayati Shujaa Nelson Mandela, amesilimu na kufunga ndoa na binti Mwislamu, Rabia Clarke.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, harusi hiyo ilifanyika wikendi iliyopita na kwamba Mandla Mandela alisilimu miezi miwili iliyopita. Nikah ya wawili hao imefungwa na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu Sheikh Ibrahim Gabriels. Mandla hivi sasa ni kiongozi wa jadi wa kabila la Xhosa katika eneo la Mvezo alikozaliwa Shujaa Nelson Mandela. Bi. Rabia Clarke alizaliwa katika familia ya Waislamu inayoishi katika mji wa Cape Town.

Akizungumza wakati wa nikha na harusi yake siku ya Jumapili, Mandla alisema: "Ni fakhari na furaha yangu kutangaza kufunga ndoa na Rabia mjini Cape Town mnamo Februari 6, 2016. Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wazazi wa Rabia, familia yote na jamii ya Waislamu kwa kunikaribisha katika nyoyo zao."

Mandla Mandela ameongeza kuwa: "Ingawa tumetoka tamaduni tafauti, lakini zina nukta za pamoja na moja ya nukta hizo ni kuwa sote tunafungamana na Afrika Kusini."

Hayati Shujaa Nelson Mandela anatambulika duniani kama kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi katika historia ya zama hizi.

Mandela alifariki dunia Desemba mwaka 2012 akiwa na umri wa miaka 95. Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alitumia zaidi ya nusu ya umri wake akipambana na utawala wa kibaguzi nchini kwake. Utawala wa wazungu wabaguzi ulimfunga jela kwa kipindi cha miaka 27 hadi mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipofutwa mwaka 1990. Mwaka 1994 wananchi wa Afrika Kusini walimchagua Mandela kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo.

3474246

captcha