IQNA

Mwanamke Mwislamu atimuliwa kazini Marekani kwa kuvaa Hijabu

10:32 - January 02, 2020
Habari ID: 3472325
TEHRAN (IQNA) – Mwanamke Mwislamu nchini Marekani ametimuliwa katika mgahawa aliokuwa akifanya kazi kwa sababu tu ya kuja kazini akiwa amevalia vazi la staha la Hijabu.

Folake Adebola amesambaza kilpu ya sekunde 45 katika Twitter inayoonyesha namna msimamizi wake katika mgahawa wa Chicken Express huko Fort Worth, Dallas alivyomtimua kazini.

Katika klipu hiyo anasikika akijitetea akisema 'vazi la hijabu ni sehemu ya dini yangu.' Katika ujumbe kupitia Twitter ameandika: "Nilisilimu hivi karibuni na nikaanza kuvaa Hijabu. Leo kimefika kazini na nimefutwa kazi wa sababu ya kuvaa Hijabu. Wamedai si sehemu ya sare za kazi. Nawatolea wito msije katika Chicken Express mjini Fort Worth."

Bi Adebola amesema kufutwa kazi kwa ajili tu ya kuvaa Hijabu ni ubaguzi wa hali ya juu.

Shirika la Chicken Express bado halijatoa taarifa kuhusu tukio hilo.

Msichana Muislamu nchini Marekani ameondolewa kwenye mashindano ya mbio za nyika kwa sababu ya kuvaa Hijabu. Noor Alexandria Abukaram mwenye umri wa miaka 16 amelaani vikali udhalilishaji na ubaguzi aliofanyiwa kwa misingi ya dini yake wakati wa mashindano ya mbio za nyika katika mji wa Findlay jimboni Ohio mapema mwezi Oktoba.

Hivi karibuni pia, askari Mwislamu wa kike katika jeshi la Marekani kwa jina Cesilia Valdovinos aliwafungulia mashtaka makamanda wake kwa kumlazimisha kuvua hijabu.

Baraza la Uhusiano wa Kiislamu nchini Marekani (CAIR) limeonya kuwa vitendo vya uhalifu vinavyotokana na chuki dhidi ya Uislamu vimeongezeka nchini humo haswa tangu Donald Trump alipoingia madarakani nchini humo.

3868121

captcha